Mamia ya raia waruhusiwa kuondoka Gaza kupitia Rafah
13 Novemba 2023Mamia ya raia wa kigeni na majeruhi wa Kipalestina wameruhusiwa kuondoka Gaza kupitia kivuko cha Rafah kilichofunguliwa tena. Chanzo kimoja katika mpaka huo upande wa Palestina, kimelieleza shirika la habari la Ujerumani la dpa kwamba watu wapatao 800 wamefanikiwa kuvuka mpaka huo na kuingia Misri.
Soma: Mashambulizi ya Israel yaendelea kutikisa Gaza
Hayo yanajiri wakati wafanyakazi wa hospitali ya Al-Shifa iliyoko Kaskazini mwa Gaza wakiripoti kuongezeka kwa mapigano. Msemaji wa jeshi la Israel IDF Richard Hecht, amekanusha ripoti za Shirika la madaktari wasio na mipaka MSF kwamba watu waliokuwa wakikimbia hospitali ya Al-Shifa huko Gaza walipigwa risasi. Hecht ameieleza DW kwamba hawawalengi raia, bali wanamgambo wa Hamas. Ameongeza kuwa hospitali ya Al-Shifa ni kitovu kikuu cha shughuli za Hamas, ambapo wanamgambo wa Hamas wamejificha ndani na pia chini ya hospitali.
Naye Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kwamba anapinga hatua ya usitishaji mapigano mara moja na kurejelea wito wa Ujerumani wa kuunga mkono usimamishaji wa muda mfupi ili kuwezesha usambazaji wa misaada ya kiutu. Ujerumani ilijizuia kupiga kura ya Umoja wa Mataifa tarehe 26 Oktoba ya kutaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.