1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia wajeruhiwa Jerusalem kufuatia makabiliano na polisi

10 Mei 2021

Mamia ya watu wamejeruhiwa Jumatatu kufuatia makabiliano kati ya vikosi vya usalama vya Israel na Wapalestina mjini Jerusalem.

https://p.dw.com/p/3tBxS
Israel | Unruhen in Jerusalem
Picha: Ammar Awad/REUTERS

Machafuko hayo yamejiri mnamo wakati maandamano yamepangwa sambamba na siku ambayo Israel ilichukua udhibiti wa mji huo mtakatifu mwaka 1967, hali inayotisha kusababisha vurugu zaidi. 

Kulingana na shirika la Hilal Nyekundu la Palestina, mamia ya watu wamejeruhiwa huku zaidi ya 50 wakilazwa tangu machafuko hayo yalipoanza Ijumaa iliyopita wakati wa ibada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Baada ya usiku uliojaa vurugu, Wapalestina waliwarushia maafisa wa usalama wa Israel mawe na vitu mbalimbali, huku maafisa hao wakijibu kwa kufyatua risasi za mipira, mabomu ya kushtua pamoja na gesi za kutoa machozi. Hayo ni kulingana na mwandishi mmoja wa habari wa shirika la habari la AFP.

Nini kiini cha mzozo wa Mashriki mwa Jerusalem?

Machafuko hayo mabaya ndiyo ya hivi karibuni kuhusu mzozo wa Jerusalem tangu mwaka 2017, ambayo imechochewa na mvutano ambao umedumu kwa mwaka mmoja wa Wayahudi walowezi kutaka kuchukua udhibiti wa makaazi ya karibu ya Wapalestina yaliyoko mashariki mwa Jerusalem, sehemu ambayo Israel ilichukuwa kwa nguvu.

Vikosi vya usalama vya Israel vyafyatua gesi za kutoa machozi kufuatia machafuko na Wapalestina katika mji mkuu wa kale wa Jerusalem Mei 10, 2021.
Vikosi vya usalama vya Israel vyafyatua gesi za kutoa machozi kufuatia machafuko na Wapalestina katika mji mkuu wa kale wa Jerusalem Mei 10, 2021.Picha: Emmanuel Dunand/AFP/Getty Images

Kesi muhimu iliyopaswa kusikizwa mahakamani leo kuhusu eneo ambalo ni kitovu cha mzozo Sheikh Jarrah mashariki mwa Jerusalem imeahirishwa.

Kiongozi wa chama cha dini ya Kizayuni chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia Bezalel Smotrich pia ametangaza kuzuru wilaya hiyo yenye machafuko ya Jarrah.

Hofu ya machafuko zaidi yatanda

Kulikuwa na wasiwasi kwamba kutatokea ghasia zaidi wakati wa maandamano yaliyopangwa na Israel kuadhimisha ushindi wao walipouchukua na kudhibiti Jerusalem mwaka 1967 baada ya vita vya siku sita. Maadhimisho ambayo huitwa Siku ya Jerusalem katika taifa hilo la Kiyahudi.

Mnamo Jumapili, polisi ya Israel iliidhinisha maandamano hayo yanayotarajiwa kufanyika leo kuanzia saa kumi jioni.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameitetea Israel kuhusu namna ambavyo imeshughulikia maandamano na vurugu hizo akisema watafuata sheria na utaratibu vilivyo na kwa uwajibikaji huku akisisitiza kuheshimu uhuru wa kuabudu kwa madhehebu yote.

Hata hivyo matendo ya Israel ya kuzidisha uhasama hususan kufuatia makabiliano katika maeneo ya Msikiti Al-Aqsa ambao ni eneo la tatu kwa utakatifu kwa Waislamu, imekosolewa vikali na wengi.

Jumuiya ya kimataifa yotoa wito wa utulivu kurejeshwa

Uturuki vilevile imetoa wito kwa Israel kukoma kuwashambulia Wapalestina.

Mataifa yote sita ya Kiarabu ambayo yana uhusiano wa kidiplomasia na Israel zikiwemo Misri, Jordan, Umoja wa falme za Kiarabu, Bahrain, Morocco na Sudan zimeishutumu Israel.

Maafisa wa polisi wa Israel waonekana wakiwa juu ya majengo wakishika doria mbele ya mji wa kale wa Jerusalem Mei 10, 2021.
Maafisa wa polisi wa Israel waonekana wakiwa juu ya majengo wakishika doria mbele ya mji wa kale wa Jerusalem Mei 10, 2021.Picha: Ilan Rosenberg/REUTERS

Tunisia imesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kuandaa kikao cha faragha Jumatatu kulingana na ombi lake, kuhusu machafuko hayo.

Mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Urusi na Marekani waliko Mashariki ya Kati, pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na vilevile mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis, wote wametaka utulivu kurejeshwa.

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema zaidi ya Wapalestina 300 walijeruhiwa kufuatia machafuko yaliyotokea usiku wa Ijumaa na Jumamosi.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF limesema watoto 29 wa Wapalestina pia walijeruhiwa kwenye machafuko hayo.

(AFPE, AP)