1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malumbano yazuka, bunge la Ujerumani

Oumilkheir Hamidou
27 Novemba 2019

Malumbano yamegubika majadiliano ya bajeti ya serikali kuu bungeni, kati ya serikali na upande wa upinzani. Mada zote ziliwasilishwa lakini Kansela Angela Merkel akijikita zaidi katika siasa ya nje na usalama. 

https://p.dw.com/p/3TqD3
Berlin Bundestag Rede Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Ikiwa imesalia wiki moja kabla ya mkutano wa kilele wa jumuia ya kujihami ya NATO kuitishwa mjini London, kansela Angela Merkel ametoa hutuba kali mbele ya wabunge mjini Berlin akitetea umuhimu wa jumuia ya kujihami ya NATO iliyoundwa mwaka 1949 na ambayo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anasema  "iko katika hali mahtuti".

Kansela Merkel ametoa wito Ujerumani iwajibike zaidi na kuahidi bajeti ya usalama itazidishwa kutoka asilimia moja nukta nne na kufikia asilimia moja nukta tano ifikapo mwaka 2024. Kuanzia mwaka 2030 bajeti ya ulinzi itafikia asilimia mbili.

Katika kikao cha majadiliano jumla bungeni kaansela Merkel amezungumzia pia jukumu la Ujerumani katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhimiza pawepo mkakati wa aina moja wa nchi za Ulaya kuelekea China. Wakati huo huo ametetea umuhimu wa kuendelezwa serikali kuu ya muungano hadi mhula wake utakapokamilika na uchaguzi mkuu kuitishwa mwaka 2021.

Berlin Bundestag Rede Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela Angela Merkel akilihutubia bunge la Ujerumani hii leo.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kinyume chake mkuu wa kundi la wabunge wa chama chaa siasa kali za mrengo wa kushoto die Linke Dietmar Bartsch anatoa wito muungano huo uvunjwe. Mwenyekiti wa chama cha kiliberali cha FDP Christian Lindner anaituhumu serikali kushindwa kuwajibika katika masuala ya kiuchumi.

Katika hotuba yake ya kusisimua kansela Merkel ameshadidia umuhimu wa jumuia ya kujihami ya NATO na kusema "Ni kwa masilahi yetu wenyewe kuiendeleza jumuiya ya kujihami ya NATO, au angalao kama ilivyokuwa wakati wa vita baridi, kwa masilahi yetu, kwasababu, kama alivyosema waziri wa mambo ya nchi za nje, Ulaya haiwezi kujitetea wenyewe,tunategemea jumuia ya kujihami ya na hiyo ndio maana ni waajibu wetu kuwajibika na kutwaa majukumu makubwa zaidi."

Katika wakati ambapo kansela Merkel alikuwa anatetea sera ya serikali yake kuhusu mabadiliko ya tabianchi, mwenyekiti wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Chaguo Mbadala kwa Ujerumani, AfD Alexander Gauland amekosoa mpango wa mageuzi ya nishati akisema utavifilisi viwanda vya magari na uhandisi.