1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali,Rwanda na Angola zachambuliwa magazetini

8 Februari 2013

Vita nchini Mali,kutakaswa mawaziri 2 wa zamani wa Rwanda na mahakama ya kimataifa ya Arusha na jinsi fedha zinavyochezewa nchini Angola ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya magazeti ya Ujerumani wiki hii.

https://p.dw.com/p/17ajn
Watoto wanapekua katika magofu ya hoteli moja iliyobomolewa na wanajeshi wa Ufaransa na Mali huko DouentzaPicha: AFP/Getty Images

Tuanzie lakini Mali ambako opereshini za kijeshi za wanajeshi wa Ufaransa wakisaidiwa na wale wa Mali zinaendelea dhidi ya wanamgambo wa kiislamu katika maeneo ya milima na jangwa kaskazini mwa nchini hiyo. "Vita bila ya picha za kuchukiza" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la "Süddeutsche" linahoji jeshi la Ufaransa na vikosi vya jeshi la serikali ya Mali wamefanikiwa kuwatenga waandishi habari na mapigano. Süddeutsche  Zeitung linasema hata hivyo mtu akiitembelea hospitali moja ya jangwani katika mji wa Sévaré hatokawia kutambua jinsi vita hivyo vinavyowaathiri pia raia wasiokuwa na hatia. Huko ndiko wanakotibiwa wanajeshi na raia waliojeruhiwa. Idadi halisi ya waliojeruhiwa haijulikani na idadi ya wahanga ndio kabisa. Gazeti hilo limelinukuu shirika la maripota wasiokuwa na mipaka likiwakosoa wanajeshi wa Ufaransa na Mali kwa kuwazuwia waandishi habari wasiyafikie maeneo ya mapigano. Shirika lisilokuwa na mipaka linasema licha ya ripoti za kukombolewa miji haraka na bila ya upinzani, Timbuktu vita vya kweli vilipamba moto, mabomu kuripuliwa na visa vya kulipiza kisasi kutokea na kusababisha wahanga kadhaa.

Gazeti la Der Tagesspiegel linazungumzia kuhusu mipango ya Ufaransa kuwaondoa wanajeshi wake kuanzia mwezi ujao wa Machi katika wakati ambapo mapigano ndio kwanza yanapamba moto. Katika wakati ambapo rais Francois Hollande akiwa ziarani nchini Mali amezungumzia kuhusu kusalia wanajeshi wa nchi yake wakati wote utakaohitajika, waziri wake wa mambo ya nchi za nje Laurent Fabius anatangaza umuhimu wa kuona operesheni za kijeshi nchini Mali zikisimamiwa na Umoja wa mataifa. Der Tagesspiegel limemnukuu mwanadiplomasia mmoja wa Umoja wa mataifa akisema baraza la usalama la umoja wa mataifa huenda likapitisha azimio kuhusu hilo hadi ifikapo mapema mwezi ujao wa Machi.

Mahakama kuu ya kimataifa yaamua

Justin Mugenzi und seine Anwälte
Justin Mugenzi (kushoto) na mawakili wakePicha: AFP/Getty Images

Lilikuwa gazeti la mjini Berlin, die Tageszeitung, lililoandika kuhusu kisa cha kuachiliwa huru mawaziri wawili wa zamani wa Rwanda, ambao awali walikutikana na hatia ya kuhusika na mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994. "Kwanza ndio wana hatia na sasa hawana" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo la mji mkuu. Linasema mahakama ya kimataifa ya uhalifu yabadili maoni yake. Katika kesi ya rufaa Jumatatu iliyopita mjini Arusha nchini Tanzania, mahakama maalumu ya kimataifa ya uhalifu wa vita vya Rwanda, ICTR, ilibatilisha hukumu iliyopitishwa Septemba 30 mwaka 2011 dhidi ya waziri wa zamani wa biashara Justin Mugenzi na waziri wa zamani wa watumishi wa serikali, Prosper Mugiraneza, waliotiwa hatiani wakati ule kwa kuchochea mauwaji ya halaiki. Kwa namna hiyo mawaziri wote wanne wa kile kilichokuwa kikijulikana kama "serikali ya mpito nambari mbili" ambao kesi yao ilianza mwaka 2003 mjini Arusha wameachiwa huru. Gazeti la Die Tageszeitung limekumbusha mahakama hiyo iliwaachia huru hapo awali waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje, Casimir Bizimungu, na waziri wa zamani wa afya,Jérôme Bicamumpaka, kwa ukosefu wa ushahidi.

Wachezeaa mali na nchi maskini

Isabel dos Santos - Unternehmerin Tochter des Präsidenten von Angola
Isabel dos Santos - binti ya rais Edouardo dos Santos wa AngolaPicha: Nélio dos Santos

"Tajiri mwenye kumiliki mabilioni katika nchi fukara" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Die Welt linalozungumzia kuhusu harusi ya mtoto wa kike wa rais wa Angola, Jose Eduardo dos Santos. Katika sherehe za harusi yake pamoja na mtoto wa tajiri mmoja wa Kongo, Sindika Dokolo, Isabel dos Santos amelileta kundi la wanamuziki wa kwaya kutoka Ubeligiji. Chakula pekee kilichotengenezwa kwa ajili ya watu elfu kumi walioalikwa kimeagiziwa na kuletwa kwa ndege mbili kutoka Ufaransa. Euro milioni tatu zimetumika kwa ajili ya sherehe ya harusi ya mtoto wa kike wa rais wa Angola ambapo waziri wa uchumi na nishati ndiye aliyechaguliwa kuwa shahidi. Harusi hiyo ya fakhari bado watu wanaizungumzia katika mji mkuu Luanda, miaka tisa baadaye. Si sifa nzuri kwa mjasiriamali huyo mwenye umri wa miaka 40 anayejaribu kubuni makampuni makubwa makubwa nchini Angola na Ureno katika wakati ambapo kwenye ripoti ya Transparency International Angola inajikuta mkiani mwa nchi zilizooza kwa rushwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/All/presse

Mhariri: Josephat Charo