1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali yaituhumu Ufaransa na kutishia kujihami

19 Oktoba 2022

Waziri wa Mambo ya nje wa Mali Abdoulaye Diop amesema serikali ya kijeshi ya nchi hiyo itatumia haki yake ya kujilinda ikiwa Ufaransa itaendelea kudhoofisha uhuru na usalama wa taifa hilo la Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/4INEC
Mali | Abdoulaye Diop
Picha: Thiam Nana Diallo

Akizungumza jana katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Mali mjini New York, Waziri Abdoulaye Diop alirejelea madai kwamba Ufaransa ilikiuka mipaka yake ya anga na kukabidhi silaha kwa Wanamgambo wa Kiislamu ambao wamekuwa wakiendesha mashambulizi kaskazini mwa Mali kwa muongo mmoja sasa.

Ufaransa imekanusha shutuma hizo wakati ambapo uhusiano wake na Mali umedorora tangu mapinduzi ya Agosti mwaka 2020 na baada ya kuwaondoa askari wake waliotumwa mnamo mwaka 2013 kusaidia kupambana na uasi.

Diop amesema kuna haja ya kuwa na mkutano maalum wa Baraza la Usalama ambao utatoa mwanga kuhusu ushahidi wa vitendo vya udadisi, ujasusi na uharibifu vinavyofanywa na Ufaransa.

Aidha Diop ameendelea kuwa serikali ya Mali yaweza kutumia haki yake ya kujilinda ikiwa Ufaransa itaendelea kudhoofisha uhuru na usalama wa taifa hilo, huku akisisitiza kuwa hatma ya Mali iko mikononi mwa raia wake:

" Watu wa Mali wameamua kuchukua hatima yao mikononi mwao. Wananchi wa Mali wanaiunga mkono kikamilifu Serikali katika mageuzi ya kisiasa na kitaasisi, katika juhudi na hatua zinazoendelea za kulinda eneo la taifa, katika ulinzi wa watu na mali zao, na katika utoaji wa huduma za msingi za kijamii. "

Ufaransa yakanusha

Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/Pool/AP/picture alliance

Mwakilishi wa Ufaransa katika UN, Nicolas De Riviève alikanusha tuhuma hizo alizozitaja kuwa "uzushi" na kubaini kuwa harakati zote ambazo Ufaransa imeendesha nchini Mali zilifanyika kwa uwazi na kusema nchi yake haijawahi kukiuka mipaka yoyote ya anga.

Katika mkutano huo, Diop alikanusha pia ripoti za Umoja wa Mataifa na makundi mengine kuhusu vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na Jeshi la Mali.

Ripoti kadhaa, ikiwa ni pamoja na tathmini ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, zinawatuhumu wanajeshi wa Mali na mamluki wa Urusi kushirikiana na serikali ya kijeshi kwa kutumia vibaya uongozi na kuwaua raia wanaoshukiwa kushirikiana na makundi ya kigaidi.

Diop alitaja madai hayo kuwa "hayana msingi" na akaonya dhidi ya "upotoshaji" katika masuala ya haki za binadamu, huku akibaini kuwa kuondoka kwa mamia ya wanajeshi wa kigeni hakutasababisha ombwe la usalama.

Uhusiano wa Mali na Urusi

Russland Mali Abdoulaye Diop  Sergey Lavrov
(Kushoto): Abdoulaye Diop, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali - (Kulia):Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Picha: Alexander Shcherbak/dpa/picture alliance

Mataifa mengine ya Ulaya yamesitisha ushiriki wao kijeshi nchini Mali mwaka huu, wakitaja kuwa utawala wa kijeshi umekuwa ukishirikiana na mamluki wa Urusi.

Wanamgambo wa Kiislamu wamesonga mbele zaidi kuelekea Mashariki mwa Mali, huku wakidhibiti maeneo kadhaa na kuwaua mamia ya raia huku maelfu ya wengine wakiyahama makazi yao.

Mali imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa utulivu tangu mwaka 2012, kufuatia makundi ya kigaidi. Ufaransa iliingilia kati kusaidia kuwaondoa. Lakini wanamgambo hao wengine wakiwa na mafungamano na makundi ya Al Qaeda na IS, wamekuwa wakijidhatiti tena na kuenea katika ukanda wa Sahel hasa maeneo ya kusini kuelekea majimbo ya pwani.