1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maali na Mauritania zaingia kwenye mvutano

14 Machi 2022

Mauritania yadai wanajeshi wa Mali wamehusika na visa vya kutoweka raia wa Mauritania katika eneo la mpaka baina ya nchi hizo mbili

https://p.dw.com/p/48SsT
Mali | Opération Barkhane
Picha: Philippe de Poulpiquet/LE PARISIEN/PHOTOPQR/MAXPPP/picture alliance

Mali imetangaza kuwapiga marufuku raia kutoka eneo la mpakani ambako raia wa Mauritania walitoweka na wanajeshi wa Mali walinyooshewa kidole kuwa ndio wahusika wa kisa hicho.

Taarifa za mitandao ya kijamii zilidai wanajeshi wa Mali walihusika na tukio hilo na kuzusha mivutano kati ya nchi hizo mbili jirani. Katika taarifa iliyotolewa Jumapili usiku baada ya Mali kuwatuma nchini Mauritania wajumbe wake, msemaji wa serikali kanali Abdoulaye Maiga alitangaza kwamba mamlaka ya jeshi imeamua kuzuia kabisa watu kutembea katika maeneo ya  msitu wa Wagadou na Gringale.

Taarifa zinazoenea kwenye mitando ya kijamii nchini Mauritania zililinyooshea kidole jeshi la Mali kwamba limehusika kuua raia katika eneo hilo la mpaka la kusini mwa Adel Bagrou mji ambao uko Kusini Mashariki mwa nchi hiyo. Serikali ya Mauritania imelituhumu jeshi hilo la Mali kwa kuendeleza mara kwa mara vitendo vya uhalifu lakini haikutowa ufafanuzi zaidi.

Militärputsch in Mauretanien
Picha: picture-alliance/ dpa

Ujumbe wa ngazi za juu ulikuweko mjini Nauakchott,mji mkuu wa Mauritania Ijumaa na Jumamosi kujaribu kutuliza msuguano huu uliozuka. Pande hizo mbili zilikubaliana kuanzisha uchunguzi wa pamoja kuhusu matukio hayo ya watu kutoweka na kuunda timu ya pamoja ya kupiga doria katika eneo la mpaka.

Jeshi la Mali lakanusha kuhusika

Kanali Maiga katika taarifa yake amesema maeneo ya Wagadou na Gringale yako katika eneo ambako jeshi la Mali limekuwa likiendesha operesheni zake za kukabiliana na makundi ya itikadi kali ya Jihadi tangu mwezi Desemba. Lakini akasisitiza misimamo iliyotolewa mwanzo na nchi yake kwamba jeshi halikuhusika na chochote katika visa hivyo vya raia wa Mauritania kutoweka.

Na pia amebaini kwamba katika tarehe zilizotolewa hakuna mwanajeshi wa kikosi hicho cha Mali FAMA aliyekuwa akishika doria kwenye maeneo hayo na kwahivyo hakuna ushahidi unaounga mkono madai yanayotolewa kuhusu uhalifu huo kufanywa na FAMA.

Weltspiegel | Bamako, Mali | Militärputsch, Protest gegen Frankreich
Picha: Michele Cattani/AFP

Visa vya kutoweka

Katika tukio jingine mwendesha mashtaka wa mahakama ya kijeshi nchini Mali mjini Bamako ametangaza kwamba uchunguzi kuhusu visa hivyo  vya watu waliotoweka utafanywa na kikosi maalum cha jeshi la Jendarmeri. Ingawa taarifa iliyotolewa haikutowa ufafanuzi zaidi ingawa inafahamika kwamba kuna matukio mawili ya watu waliotoweka moja likiwa limeripotiwa mnamo mwezi Januari na jengine mwanzoni mwa mwezi Machi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW