1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali kutumia ''kila njia'' kuikomboa kaskazini

Admin.WagnerD17 Julai 2012

Waziri Mkuu wa Mali Cheick Modibo Diarra, amesema serikali yake inaangalia uwezekano wa kuanzisha operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wenye mafungamano na al Qaida, ambao waliteka eneo kubwa la kaskazini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/15YvR
Wanamgambo wa kiislamu kaskazini mwa Mali
Wanamgambo wa kiislamu kaskazini mwa MaliPicha: Reuters

Waziri Mkuu Cheick Modibo Diarra aliutangaza mpango huo kupitia televisheni ya taifa. Cheick Diarra alisema wanategemea kupata pendekezo kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Magharibi, ECOWAS, juu ya matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya waasi wanaoshikilia eneo kubwa la kaskazini. Tayari ujumbe wa ECOWAS umekwishaitembelea Mali, na jumuiya hiyo imeahidi kutoa askari 3000 kuisaidia kijeshi nchi hiyo. ECOWAS imesema inasubiri mwaliko rasmi kutoka Mali, na pia ruhusa kutoka Umoja wa Mataifa.

Lakini pia mlango umeachwa wazi kwa makundi ya kiislamu yanayolishikilia eneo hilo la kaskazini. Umoja wa Afrika umesema makundo hayo yanaweza kushirikishwa katika kutafuta muafaka wa kisiasa, iwapo yatavunja uhusiano na al-Qaida.

Serikali ya umoja wa taifa

Waziri Mkuu wa Mali Cheick Modibo Diarra
Waziri Mkuu wa Mali Cheick Modibo DiarraPicha: picture-alliance/dpa

Katika kikao chao mjini Addis Ababa wiki hii, viongozi wa kiafrika waliunga mkono mazungumzo yatakayojaribu kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ambayo inajumuisha makundi yote.

Eneo kubwa la kaskazini mwa Mali liliangukia mikononi mwa waasi kufuatia pengo la uongozi lililojitokeza baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Machi. Tangu wakati huo, eneo kubwa ambalo linajumuisha miji ya Gao, Kidal na Timbuktu linathibitiwa na makundi yanayotaka kujitenga. Makundi hayo ni pamoja na Ansar Dine la wapiganaji wa kabila la Tuareg, wanaoongozwa na Iyad Ag Ghali.

Hata hivyo, sambamba na diplomasia, Umoja wa Afrika pia unaunga mkono mpango wa ECOWAS, ambao iwapo utapata kibali cha Umoja wa Mataifa, utaanzisha operesheni za kijeshi kuwatimua waasi hao iwapo mazungumzo ya kisiasa yatakwama. Akizungumza pembeni mwa mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, kamishna wa umoja huo anayehusika na masuala ya amani na usalama, Ramtane Lamamra, alisema njia zote za kutaka kuusuluhisha mgogoro huo kisiasa hazijashindwa.

Lamamra alikaribisha hatua ya chama cha watuareg, MNLA, kuachana na madai yake ya kujitenga na kuunda taifa jipya lijulikanalo kama Azawad, baada ya mapambano ya chama hicho kutekwa nyara na makundi ya kiislamu yenye uhusiano na al-Qaida.

Zuma ataka mizozo isuluhishwe haraka

Kikao cha AU mjini Addis Ababa
Kikao cha AU mjini Addis AbabaPicha: picture-alliance/dpa

Hata rais mpya wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika, Bi Nkosazana Dlamini Zuma, katika hotuba yake ya kwanza tangu achukue wadhifa huo, alisema ataanza mara moja kushughulikia mizozo barani Afrika. Aliongeza kwamba Umoja wa Afrika umeanzisha baraza lake la usalama, kwa sababu mara nyingi Umoja wa Mataifa umekuwa ukijivuta katika kusuluhisha mizozo barani humo.

Wapiganaji wa kundi la Ansar Dine hivi karibuni waliwachapa viboko hadharani watu waliowatuhumu kuwa wazinzi katika miji waliyoiteka, na kuvunja sehemu takatifu za kiislamu katika mji wa Timbuktu ambazo zilikuwa kwenye orodha ya turathi za kimataifa.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya pia umeahidi kutuma wataalamu wake katika nchi jirani ya Niger kulipatia mafunzo jeshi la nchi hiyo juu ya mbinu za kupambana na al-Qaida. Nchi zinazounda Umoja wa Ulaya, jumatatu ziliafiki mpango wa kutumwa wataalamu hao, ambao kazi yao inategemewa kuanza rasmi mwezi ujao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE

Mhariri:Miraji Othman