Makundi hasimu yauwa watu 27 Tripoli
16 Agosti 2023Mapigano hayo yaliyoanza ghafla jioni ya Jumatatu (Agosti 14) yaliendelea hadi jioni ya jana na, kwa mujibu wa Kituo cha Huduma ya Matibabu ya Dharura, yaliwahusisha wanamgambo wa kikosi kiitwacho 444 na mahasimu wao wa Kikosi Maalum.
Hata hivyo, kituo hicho hakikutaja ikiwa waliouawa na kujeruhiwa ni wanamgambo pekee au miongoni mwao wamo pia raia wa kawaida.
Soma zaidi: Mapigano makali yazuka kati ya makundi hasimu mjini Tripoli
'Libya: Hali tete raia wenye hasira waandamana kupinga ugumu wa maisha
Vyombo vya habari nchini humo vinasema mzozo ulianza baada ya kamanda mmoja wa ngazi za juu wa kundi la 444, aitwaye Mahmoud Hamza, kukamatwa na mahasimu wao kwenye uwanja wa ndege wa Tripoli mapema siku ya Jumatatu.
Wakati mapigano yakiendelea, wizara ya afya ya Libya iliyaomba makundi hayo hasimu kuruhusu timu za uokozi na magari ya dharura kuingia kwenye maeneo ya mapigano, hasa kusini mwa mji wa Tripoli, na pia ilitowa wito wa msaada wa damu kwenye hospitali za karibu na maeneo hayo.
Shirika linalohusika na usafiri wa anga nchini humo limesema kuwa ndege nyingi ziliondoka mjini Tripoli tangu jioni ya Jumatatu kutokana na mapigano hayo na kwamba ndege zilizokuwa zituwe kwenye uwanja huo zilihamishiwa kwenye uwanja wa ndege wa mji wa Misrata.
Libya yaendelea kugawanyika
Mapigano hayo yalitokea baada ya miezi kadhaa ya utulivu kufuatia muongo mzima wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya, ambako mamlaka mbili hasimu zimekwama kwenye mkwamo wa kisiasa.
Migawanyiko ya muda mrefu imechochea mapigano ya mara kwa mara mjini Tripoli katika miaka ya hivi karibuni, ingawa takribani yote hudumu kwa masaa machache na kumalizika, lakini ni baada ya kujeruhi na kuangamiza maisha ya watu kadhaa.
Soma zaidi: Libya yazama katika bahari ya damu
Wageni wazidi kuhamishwa kutoka Libya
Siku ya Jumanne (Agosti 15), Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo ulisema unafuatilia mzozo ambao umezusha khofu kwa usalama na maendeleo yaliyopigwa ndani ya kipindi hiki, na ukatowa wito wa pande zote kuacha mapigano mara moja.
Mamlaka zote mbili hasimu zinazotawala Libya pia zililaani mapigano hayo kupitia taarifa zao.
Baraza la Wawakilishi, ambalo lina makaazi yake kwenye mji wa mashariki wa Benghazi, liliishutumu serikali yenye makao yake mjini Tripoli kwa kuhusika na mapigano hayo.
Mapigano mapya yazuka Libya watu 40 wauawa
Mapigano yautingisha mji wa Tripoli
Balozi za Marekani na Uingereza nchini Libya zilitowa taarifa ya kuelezea wasiwasi wao juu ya mapigano hayo, huku Marekani ikitowa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama "ili kudumisha mafanikio ya hivi karibuni kuelekea uchaguzi."
Libya, taifa lenye utajiri mkubwa wa mafuta, limegawanyika tangu mwaka 2014 baina ya serikali iliyoko mashariki na ile iliyoko magharibi, kila moja ikiungwa mkono na makundi yenye silaha nzito nzito na serikali za mataifa ya kigeni, zinazotuhumiwa na wachambuzi wa mambo kwa kuiibia nchi hiyo rasilimali zake.
Vyanzo: AFP, AP