1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makaburi ya Jumla yagunduliwa

24 Desemba 2013

Umoja wa Mataifa unazungumzia kugundulika kaburi la pamoja likiwa na maiti 75 katika jimbo la Unity na Juba,wakati baraza la usalama likisubiriwa kuamua juu ya suala la kuongezwa wanajeshi nchini humo

https://p.dw.com/p/1AgST
Picha: Reuters

Taarifa zilizotolewa hivi punde zinazungumzia kugunduliwa kaburi la jumla jamala lililokuwa na maiti za watu 75 katika jimbo la Unity na mengine mawili yamegunduliwa kwenye mji wa Juba baada ya ghasia za kikabila.Taarifa hizo zimetangazwa na Umoja wa Mataifa na kufuatia na wito wa kamishna mkuu wa Umoja huo anayesimamia masuala ya haki za bindamu Navi Pillay wa kutaka pande zote kuwalinda raia na kuonya kwamba viongozi wa kisiasa na kijeshi huenda wakabebeshwa dhamana ya uhalifu huo. Hata hivyo msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Kanali Phillip Aguer anasema jeshi halihusiki na ikiwa wapo wanaohusika watachukuliwa hatua.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture alliance/abaca

Taarifa hizo za kugunduliwa makaburi ya pamoja zinakuja saa chache kabla ya wanachama 15 wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kukutana kupiga kura kuamua ikiwa linaridhia kuongezwa kwa kikosi chake cha kulinda amani Sudan Kusini.Idadi ya wanajeshi wanaotakiwa kuongezwa ni 5,500 kwa mujibu wa balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo UNMISS tayari una wanajeshi 7000,polisi na wafanyakazi wanaohusika na masuala ya kiraia ambapo wanajeshi wengi wa kulinda amani wa kikosi hicho wakiwa ni kutokea zaidi India.Kutokana na hilo haifahamiki wanajeshi watakaoongezwa watatokea katika nchi gani.Katibu mkuu wa Umoja huo Ban Ki Moon aliyetowa pendekezo hilo na kuitisha kikao maalum cha baraza la usalama kutafakari azimio hilo ameashiria jana Jumatatu kwamba walinda amani wa Umoja huo katika baadhi ya nchi za Kiafrika huenda wakapelekwa Sudan Kusini.

Wakati huohuo mjumbe wa Marekani katika Sudan Kusini Donald Booth amesema baada ya kukutana na rais Salva Kiir mjini Juba kwamba yuko tayari kuanza mazungumzo na Riek Machar kwa lengo la kuumaliza mgogoro bila ya masharti yoyote pindi hasimu wake atakaporidhia hilo.Machar alitimuliwa na Kiir kama makamu wake mwezi Julai na tangu wakati huo hali ya kisiasa imekuwa ya vuta nikuvute ndani ya taifa hilo.

Wanajeshi wa Sudan Kusini wamegawika makundi mawili
Wanajeshi wa Sudan Kusini wamegawika makundi mawiliPicha: Getty Images

Machar lakini anaarifiwa pia kuridhia mazungumzo na Kiir.Makundi yanayohasimiana ndani ya jeshi la serikali yamekuwa yakipambana tangu Desemba 15 na mamia ya watu wameuwawa wakati nchi hiyo ikionekana kuelekea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.Rais Kiir anamtuhumu Machar kujaribu kupanga mapinduzi huku Machar akisema Kiir amegeuka kuwa dikteta na kuweka wazi kwamba ni kweli ana nia ya kumuondowa rais huyo madarakani na kuitwaa nafasi hiyo.

Kiir anatokea kabila la Dinka,kabila ambalo ndio kubwa kabisa nchini humo wakati Machar akiwa wa kabila la Nuer.Kiasi watu 500 wamepoteza maisha katika kipindi cha wiki moja iliyopita na kutokana na hilo Katibu mkuu Ban Ki Moon ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti ya mauaji ya kikabila .Mamia kwa maelfu ya watu wameachwa bila makaazi ikiwa ni pamoja na raia 45,000 waliokimbilia hifadhi katika kambi za Umoja wa Mataifa nchini humo.

Mwandishi :Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed AbdulRahman