1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makaburi 751 yagunduliwa nchini Canada

25 Juni 2021

Zaidi ya makaburi 750 yamepatikana karibu na shule ya zamani ya bweni ya watoto wa kiasili wa Canada katika eneo la magharibi mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3vWnH
Kanada I Remembrance Day
Picha: Darryl Dyck/The Canadian Press/AP/picture alliance /

Zaidi ya makaburi 750 yasiokuwa na alama yamepatikana karibu na shule ya zamani ya bweni ya watoto wa kiasili wa Canada katika eneo la magharibi mwa nchi hiyo, hii ikiwa ni mara ya pili kwa makaburi kama hayo kugunduliwa chini ya muda wa mwezi mmoja. 

Kugunduliwa kwa makaburi hayo kwa mara nyengine kunaitia doa historia ya Canada, na kufufua miito kwa kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis kuomba msamaha kwa vitendo vya unyanyasaji katika shule hizo, ambapo wanafunzi walilazimishwa kwa nguvu kuachana na tamaduni zao za jadi.

Soma zaidi: Trudeau alaani shambulizi dhidi ya jamii ya Waislamu Canada

Kiongozi wa watu wa jamii za asili Cadmus Delorme amewaambia waandishi wa habari kuwa, wamegundua makaburi 751 yasiokuwa na alama katika shule ya zamani ya bweni ya Marieval ilioko katika mkoa wa Saskatchewan.

"Kiongozi wa kanisa katoliki anahitaji kuomba msamaha kwa kile kilichotokea katika shule ya Marieval, manusura kutoka Cowessess First Nation na kizazo chao."

Uchunguzi katika shule ya Marieval, ilioko takriban kilomita 150 mashariki mwa mji mkuu wa mkoa wa Regina, ulianza mwishoni mwa mwezi Mei baada ya kupatikana kwa miili ya wanafunzi 215 wakaazi asilia wa Canada katika shule nyengine ya zamani katika mkoa wa British Columbia.

Naye balozi wa Canada katika Umoja wa Mataifa Leslie Norton amesema,

"Kilichotokea Kamloops sio tukio la kipekee. Kwa miongo kadhaa, maelfu ya watoto wa kiasili walichukuliwa shule na kuteswa. Tunakubali kuwa Canada imekataa kukiri kuhusika na ukiukaji wa haki za watu wa asili. Lakini kama alivyosema Waziri Mkuu Justin Trudeau hivi karibuni, tunakubali kuwa watu wa asili bado wanakabiliwa na ubaguzi. Tunafahamu kuwa duniani inatarajia kuwa Canada itaheshimu sheria za kimataifa juu ya haki za binadamu. Pia sisi, tunapaswa kuheshimu sheria hizo."

Hadi miaka ya 1990, watoto wa asili ya Marekani, Metis na Inuit walilazimishwa kwa nguvu kujiunga na shule 139 zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Canada ambapo walitenganishwa na familia zao, lugha na hata kulazimishwa kuachana na tamaduni zao.

Kwa mujibu wa tume ya ukweli na maridhiano ya Canada, ni kuwa watoto wengi kutoka jamii za asili walikuwa wahanga wa unyanyasaji wa kingono huku zaidi ya 4,000 wakifariki wakiwa shule.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alisema matokeo ya uchunguzi wa tume hiyo ni mfano wa ukumbusho wa aibu wa kibaguzi, na dhulma dhidi ya watu wa jamii za asili.