1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Msumbiji yatumia nguvu kutawanya maandamano

3 Novemba 2024

Polisi nchini Msumbiji walifyatua gesi ya kutoa machozi na risasi za mpira Jumamosi, walipokuwa wakitawanya maandamano katika miji kadhaa kuhusiana na uchaguzi wa rais uliozusha mabishano.

https://p.dw.com/p/4mXoF
Waandamanaji Msumbiji
Waandamanaji Msumbiji wakionesha ujumbe katika bango huku polisi ikizuia maandamano.Picha: Alfredo Zuniga/AFP

Tangu uchaguzi mkuu wa Oktoba 9, 2024, Msumbiji imekumbwa na machafuko makubwa. Chama tawala cha Frelimo, kilichokuwa madarakani tangu 1975, kilitangazwa kushinda uchaguzi huo, lakini vyama vya upinzani vinapinga matokeo vikidai kulifanyika udanganyifu.

Watazamaji wa uchaguzi, wakiwemo wa Umoja wa Ulaya, wamebaini ukiukaji na kukosoa vurugu zilizotokea kabla, wakati, na baada ya uchaguzi.

Mgombea mkuu wa upinzani, Venancio Mondlane, ameitisha maandamano ya kitaifa kuanzia Oktoba 31 hadi Novemba 7, huku mkutano wa mwisho ikitarajiwa kufanyika Maputo.

Siku ya Jumamosi, mamia ya watu waliokuwa wamekusanyika kuandamana dhidi ya matokeo ya uchaguzi mjini Maputo walitawanywa na polisi kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi za mpira, kwa mujibu wa maripota waliokuwa kwenye eneo la tukio.

Soma pia:Machafuko yaendelea kushuhudiwa Msumbiji

Polisi walionekana wakifanya doria mjini siku ya Jumamoisi kujaribu kuwashawishi wakaazi kutoka maeneo mengine ya nchi wasije kwenye maandamano ya wiki ijayo.

Katika mkoa wa kaskazini wa Nampula, karibu kilomita 2,000 kutoka mji mkuu, makabiliana yalizuka katika maeneo kadhaa siku ya Jumamosi kati ya waandamanaji na polisi, shuhuda mmoja na kundi la ndani waliiambia AFP.

Katika mji wa Nampula, "majira ya saa tatu asubuhi, karibu watu 500 waliingia mtaani katika barabara ya Trabalo kupinga matokeo ya uchaguzi," alisema Constantino Jose, dereva tekisi mjini humo.

"Wapinzani pia walikusanyika katika Arresta (soko kubwa zaidi mkaoni Nampula) na kuzuia barabara kadhaa," alisema Jose. "Polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi na risasi halisi ili kutawanya umati wa watu," aliongeza, bila kutoa maelezo zaidi.

Polisi wajibu kwa machafuko na vizuizi vya mtandao

Shirika la kiraia la eneo hilo, Plataforma Decide, liliiambia AFP kwamba "mkoa wa Nampula uko katika machafuko" na kwamba "katika Jiji la Nampula... polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi." Polisi hawakujibu ombi la AFP la kuzungumzia ripoti hizo.

Katika mji wa Namialo, takriban kilomita 95 kutoka Nampula, "zaidi ya waandamanaji mia moja walichoma matairi barabarani," alisema mwandishi wa habari wa eneo hilo, akiongeza kwamba "kikosi cha polisi chenye nguvu" kilikuwa kimepelekwa katika eneo hilo.

Wimbo ´Supa Woman´ waibua harakati za wanawake Msumbiji

Aliomba kutotajwa jina kwa sababu ya hofu ya usalama wake. Chanzo kingine kilisema kwamba watu wasiopungua tisa walikuwa wamepigwa risasi, lakini haikuwa wazi mara moja kama ni risasi za gesi ya kutoa machozi au risasi za moto.

Afisa mmoja wa eneo hilo, Melchior Focas, msimami katika eneo la Meconta-Namialo, alithibitisha kwa AFP kwamba kulikuwa na "makabiliano" katika eneo hilo.

Msumbiji imeweka vizuizi vya mtandao tangu kuzuka kwa ghasia baada ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuzuia upatikanaji wa Facebook, Instagram na WhatsApp. Mondlane amekuwa akitumia sana majukwaa ya mitandao ya kijamii kuwasiliana na wafuasi wake na kuwaalika kuandamana.

Soma pia:Chama kikuu cha upinzani nchini Msumbiji chaomba kura kuhesabiwa upya

Machafuko yalianza muda mfupi baada ya uchaguzi, na kugeuka kuwa wa vurugu mnamo Oktoba 24 wakati tume ya uchaguzi ilipomtangaza Daniel Chapo wa Frelimo, mwenye umri wa miaka 47, kuwa mshindi kwa asilimia karibu 71 ya kura.

Mondlane, mwenye umri wa miaka 50, kutoka chama kidogo cha Podemos, alishika nafasi ya pili kwa asilimia 20 lakini alisema matokeo hayo ni "ya uongo".

Polisi wamesema watu 20 wamejeruhiwakatika ghasia za baada ya uchaguzi na kwamba watu wawili wamefariki, bila kutoa maelezo zaidi. Uchunguzi umeanzishwa dhidi ya Mondlane kufuatia machafuko hayo na wito wake wa "siku 25 za kuogofya."