1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majaji wa ICC wamuachia huru Gbagbo

Sekione Kitojo
15 Januari 2019

Katika hukumu ambayo ni pigo kwa waendesha mashitaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC, majaji wamemuachia huru rais wa zamani wa Cote d’Ivoire Laurent Gbagbo na waziri wa zamani wa vijana Cherles Ble Goude.

https://p.dw.com/p/3Bayg
Kombibild - Charles Blé Goudé und Laurent Gbagbo
Charles Ble Goude (kushoto) Laurent Gbagbo (kulia)

Majaji hao, wakimvua  dhamana  ya  jukumu  la  uhalifu  uliotokea  kufuatia mzozo  wa  uchaguzi  mwaka  2010, wakisema  upande  wa mashitaka  ulishindwa  kutoa  ushahidi  wa  kesi  hiyo.

Niederlande Laurent Gbagbo vor dem Internationalen Straferichtshof in Den Haag
Rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent GbagboPicha: Reuters/P. Dejong

Jaji Cuno Tarfusser  aliamuru  kuachiwa  huru  mara  moja  kwa kiongozi  huyo  wa  zamani  mwenye  umri  wa  miaka  73 Gbagbo pamoja  na  Ble Goude  mwenye umri  wa  miaka  47  kufuatia hukumu  hiyo  ambayo  imekuja  kabla  ya  mawakili  wao kutoa utetezi. Tarfusser  amesitisha  amri  hiyo  kabla  ya  kikao  cha ufuatiliaji  hapo  kesho Jumatano.

Waendesha  mashitaka  wanaweza  kukata  rufaa. Katika  taarifa  ya maandishi , wameieleza  hukumu  hiyo  kuwa  "inakatisha  tamaa  na isiyotarajiwa" na  kusema  watafanya  tathmini  uamuzi  huo  ulioko katika  maandishi wakati  utakapochapishwa "na  kutathimini  hatua muafaka za  kuchukua."

Gbagbo  alikuwa  rais  wa  kwanza  wa  zamani  kufikishwa  katika mahakama  hiyo  ya  dunia  na  kesi  yake  ilionekana  kama alama muhimu  katika  juhudi  za  kuwafikisha   katika  mikono  ya  sheria viongozi  wa  ngazi  za  juu  wanaoshutumiwa  kufanya  mauaji.

Elfenbeinküste Alassane Ouattara politischer Rivale von Laurent Gbagbo
Rais wa sasa wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara (kushoto)Picha: DW/K. Gänsler

Waendesha  mashitaka washindwa kuthibitisha 

Zaidi  ya  watu 3,000 waliuwawa  baada  ya  Gbagbo  kukataa kukubali  kushindwa  na  hasimu  wake  na  rais  wa  sasa  wa  Cote d'Ivoire Alassane Ouattara.

Tarfusser  amesema wengi miongoni  mwa  majaji  watatu  katika jopo  la  majaji   katika  kesi  hiyo  wameamua kwamba "waendesha mashitaka  wameshindwa  kuthibitisha mzigo wa  jukumu  dhidi  ya watu  hao  wawili.

"Mahakama  baada  ya  kufanya  tathmini  ya  kina kuhusu ushahidi na  kutafakari  kuhusu  maelezo  yote  yaliyowasilishwa kwa  mdomo na  kwa  maandishi  kutoka  pande  zote na  walioshiriki, imegundua kwa  wingi  wa  majaji kwamba  hakuna  haja  kwa  upande  wa utetezi kuwasilisha ushahidi  zaidi  kwa  kuwa  waendesha mashitaka  wameshindwa  kutoa  maelezo  ya  kutosheleza  kuhusu ushahidi wa  uhusiano  wa  mambo  mbali  mbali  yahusuyo  uhalifu kama ulivyowekwa  katika  mashitaka."

Krise in der Elfenbeinküste
Ghasia kubwa zilitokea nchini Cote d'Ivoire mwaka 2010 baada ya uchaguziPicha: picture-alliance/dpa

Jaji Tarfusser  amesema  ni  muhimu  kuweza  kumbukumbu kwamba Cote d'Ivore  ilivurugwa  na  ghasia  za  baada  ya  uchaguzi  mwaka 2010  na  mapema  2011, lakini  alisema  waendesha  mashitaka hawakuweza  kuwasilisha  ushahidi  kwamba  Gbagbo  na  Ble Goude walitayarisha  mpango  kwa  waungaji  wao  mkono  kufanya ghasia  ili  kumuweka  Gbagbo  madarakani.

Gbagbo  na  Ble  hawakuzungumza  mahakamani na  wakili  wa Gbagbo Emmanuel Altit  aliuita  kuwa  ni  ushindi  kwa  sheria.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape

Mhariri: Iddi Ssessanga