1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Ujerumani yamhukumu afisa wa zamani wa Syria

Sylvia Mwehozi
24 Februari 2021

Mahakama ya hapa Ujerumani imemhukumu miaka minne na nusu gerezani, afisa wa zamani wa idara ya usalama ya Syria kwa makosa dhidi ya ubinaadamu aliyoyatenda nchini mwake

https://p.dw.com/p/3pmoj
Koblenz Oberlandesgericht Al-Khatib Prozess
Picha: Thomas Lohnes/Pool/AFP

Afisa huyo wa zamani wa idara ya usalama ya Syria, Eyad A., amehukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu jela kwa mashitaka ya kusaidia na kuhimiza uhalifu dhidi ya binadamu. Eyad mwenye umri wa miaka 44 anatuhumiwa kuwakusanya watu kufuatia maandamano ya kupinga serikali katika mji wa Syria wa Douma mwaka 2011 na kisha kuwapeleka kwenye kituo cha mahabusu ambapo waliteswa.

Hukumu ya leo katika mahakama ya mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Koblenz inaashiria mahakama ya kwanza nje ya Syria kutoa uamuzi juu ya mateso yaliyofadhiliwa na serikali na utawala wa Rais Bashar al Assad wa Syria. Wanaharakati wa haki za binaadamu wana imani kuwa uamuzi huo utakuwa mfano kwa kesi nyingine.

Waendesha mashitaka wamedai kuwa Eyad A. aliwachukua waandamanaji wapatao 30 waliokuwa wakipinga serikali hadi kwenye gereza la siri karibu na mji wa Damascus. Gereza hilo linajulikana kama Al Khatib ama tawi nambari 251 na kisha kuwatesa waandamanaji hao mwaka 2011. Waendesha mashitaka walikuwa wakitarajia kutoa hukumu ya miaka mitano jela.

Koblenz Oberlandesgericht Al-Khatib Prozess
Mshitakiwa Eyad akiwa ameficha uso wake mahakamaniPicha: Thomas Lohnes/AFP

Upande wa utetezi uliomba kuachiliwa huru kwa mshitakiwa, ukidai kwamba mteja wao angeweza kuuawa endapo asingefuata amri. Upande huo umeongeza pia kwamba Eyad A. alisaidia tu kukamatwa watu waliokuwa wakipinga utawala wa Syria, lakini hakutimiza maagizo ya mkuu wake ya kuwapiga risasi. Wengi wanajiuliza kwanini kesi hiyo ilisikilizwa katika mahakama ya Ujerumani?

Mwaka 2012 Eyad A. alikimbia na kuondoka Syria mwaka mmoja baadae. Alikaa Uturuki na Ugiriki kwa muda na hatimaye aliwasili Ujerumani mwaka 2018, ambapo aliweza kutambuliwa na baadhi ya wahanga aliowatesa ambao wengi walikuwa wamekimbilia Ujerumani kama wakimbizi. Alikamatwa mwaka 2019 sambamba na afisa mwingine wa zamani wa ngazi ya juu Anwar R, ambaye pia kesi yake inasikilizwa mjini Koblenz.

Katika kuisikiliza kesi hiyo waendesha mashitaka wa Ujerumani walitumia kanuni za mamlaka ya sheria za kimataifa, ambayo inaruhusu uhalifu wa kivita uliofanywa na wageni kushitakiwa katika nchi zingine. Kesi dhidi ya Anwar R. bado inaendelea na uamuzi unatarajiwa kutolewa mwezi Oktoba. Afisa huyo mwenye umri wa miaka 58 alikuwa moja ya mabosi wa Eyad A. na alikamatwa Ujerumani mwaka 2019. Anakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kuratibu ukatili dhidi ya wafungwa karibu 4,000 kwenye jela ya Al Khatib kati ya mwaka 2011 na 2012 na kusababisha vifo vya watu 58.