1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Mahakama ya Rwanda yaamuru Kazungu kuzuiliwa kwa siku 30

27 Septemba 2023

Mahakama nchini Rwanda imetoa amri ya mshukiwa wa mauaji ya kupanga kuzuiliwa na vyombo vya usalama kwa siku 30 akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake baada ya miili kadhaa kukutwa imefukiwa katika shimo moja jikoni kwake.

https://p.dw.com/p/4Wr54
Flagge von Ruanda
Picha: Carl Court/AFP/Getty Images

Kesi ya Dennis Kazungu aliye na miaka 34, imewashitua wengi nchini Rwanda, hali iliyosababisha mamia ya watu kukusanyika nje na ndani ya mahakama mjini Kigali wakiwemo jamaa na marafiki za walioathiriwa. Wiki iliyopita Kazungu alikiri mashitaka yaliyomkabili wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake, akisema aliwaua watu hao 14 kwa sababu walimuambukiza kwa maksudi virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa UKIMWI.  

Jaji aliyesimamia kesi hiyo amesema Kazungu hakuonesha dalili yoyote ya kujutia matendo yake na amekubali kuhusika na uhalifu huo kwa hiyo ameamuru aendelee kuzuiliwa kwa siku nyengine 30.

Mshukiwa huyo aliyekuwa amefungwa pingu mkononi, alizomewa alipokuwa anashuka katika gari la polisi lililomleta mahakamani huku maafisa wawili wa polisi wakimuingiza ndani ya mahakama hiyo. Mmoja wa jamaa za wahanga wa mkasa huo aliondolewa mahakamani baada ya kuanza kumtusi Kazungu kwa kumuita mbwa na kumuuliza ni kwa nini alimuua binti yake.

Nadine Ahishakiye alisema hakuna kitu wanachokitaka zaidi kama haki, akisisitiza kuwa familia yake inataka haki kwa mauaji ya  dada Phanny Tuyizere, aliyekuwa na miaka 27.

Dennis Kazungu alikamatwa mapema mwezi huu baada ya polisi kugundua miili 12 katika shimo kubwa jikoni kwake mjini Kigali alikokuwa anaishi peke yake. Lakini waendesha mashtaka wamesema wiki iliyopita alikiri kuwauwa watu 14 wanawake na mwanamume mmoja. Miili ya watu wengine wawili haikupatikana. Amesema alijifunza namna ya kuwauwa watu hao wengi wao wakiwa makahaba baada ya kuangalia filamu kuhusu mauaji ya kupanga.

Waendesha mashitaka hao wamesema Dennis alitumia jina la mwanaume mmoja wa kipekee aliyekuwa katika orodha ya waliouwawa kuwauwa wanawake wengine 13. Wiki iliyopita mshukiwa huyo aliiomba mahakama kutoacha kesi yake kusikilizwa hadharani ombi ambalo mahakama ililitupilia mbali.

Kazungu aliwahi kukamatwa mwezi Julai kwa madai ya wizi na ubakaji; lakini kaachiwa kwa dhamana kufuatia kukosekana kwa ushahidi dhidi ya makosa hayo. Kulingana na vyombo vya habari Rwanda, Kazungu amewahi kufanya kazi mahali kwingi na amewahi pia kuwa mwalimu wa Kingereza nchini humo.

Chanzo: afp