1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Mahakama Uingereza yabatilisha kupeleka wakimbizi Rwanda

Hawa Bihoga
15 Novemba 2023

Mahakama ya Juu nchini Uingereza imeutupilia mbali mpango tata wa serikali wa kuwapeleka wahamiaji nchini Rwanda, na kuuridhia uamuzi wa mahakama ya chini kwamba mpango huo ni kinyume cha sheria.

https://p.dw.com/p/4YqMq
Waandamanaji wakipinga sera ya Uingereza kuwapeleka wahamiji Rwanda
Waandamanaji wakipinga sera ya Uingereza kuwapeleka wahamiji RwandaPicha: Niklas Halle'n/AFP/ Getty Images

Jopo la Majaji watano katika Mahakama ya Juu nchini Uingereza limewaunga mkono kwa kauli moja majaji wa mahakama ya Rufaa kwamba sera hiyo tata haikubaliani na wajibu wa Uingereza chini ya mikataba ya kimataifa.

Katika hukumu yenye kurasa 56, majaji walikubali kwamba Rwanda inakabiliwa na hatari ya kuwarejesha kwa lazima waomba hifadhi na wakimbizi katika nchi ambayo wanaweza kukabiliwa na mateso.

Chama tawala cha Waziri mkuu Rish Sunak cha Conservative kimesisitiza kwamba mpango huo ni muhimu katika kuhakikisha inapunguza "uhamiaji haramu" suala ambalo limewekwa wazi hata katika uchaguzi ujao.

Lakini maamuzi ya mahakama ya Juu inautupilia mbali mpango uliosainiwa kati ya Rwanda na Uingereza mnamo mwezi April mwaka uliopita wa kuwapeleka wahamiaji wasio na vibali katika vituo vya muda kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.

Waziri Mkuu Rishi Sunak amewaambia wabunge baada ya uamuzi wa mahakama kwamba serikali ya Uingereza tayari imekuwa ikiufanyia kazi mkataba mpya na Rwanda na inaweza kubadilisha sheria za nchi hiyo baada ya Mahakama ya Juu kuamua kuwa mpango wa kupeleka wahamiaji Rwanda haukuwa halali.

Soma pia:Uingereza: Tutafuata sera yetu kuwapeleka wahamiaji Rwanda

Alisema iwapo itabainika kwamba mifumo yote ya kisheria nchini na mikataba ya kimataifa bado ni ya kukatisha tamaa serikali ipo tayari kufanya marekebisho katika sheria.

"Nipo tayari kubadili sheria zetu na kupitia upya mahusiano hayo ya kimataifa."

Aliongeza kuwa waingereza wanahitaji serikali yao ichukue hatua kuzuia uhamiaji haramu na hivi ndivyo serikali inataka kulifanya.

Rwanda: Hatukubaliani na uamuzi wa mahakama Uingereza

Kufuatia maamuzi hayo ya Mahakama ya Juu ya Uingereza wa kutupilia mbali mpango wa London kupeleka wahamiaji katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa msingi kwamba haikuwa mahali salama kwa wanaotafuta hifadhi, Kigali kwa upande wake imesema inapingana na uamuzi huo kwamba Rwanda si nchi ya tatu salama kwa wanaotafuta hifadhi na wakimbizi.

Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Trinidad Express Newspaper/AFP

Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo katika tamko lake alisema Rwanda imekuwa ikijizatiti katika kutekeleza majukumu yake kimataifa ikiwa ni pamoja na"kuwapokea na kuwatendea kwa mfano wakimbizi"na kutambuliwa na shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa mataifa UNHCR pamoja na mashirika mengine ya kimataifa.

Ushirikiano wa Uhamiaji na Maendeleo ya Kiuchumi kati ya Rwanda na Uingereza unatazamia kumpeleka Rwanda mtu yeyote ambaye amefanya kile ambacho serikali inakiita "safari za hatari au zisizo halali, ikiwa ni pamoja na kusafiri kwa njia haramu ya mashua ndogo au malori ili kuingia Uingereza, mpango ambao umepingwa vikali ndani na nje ya Uingereza.

Soma pia:Viongozi wa AU wajadili mizozo, tatizo la uhamiaji na miradi ya maendeleo

Mnamo mwezi Juni mwaka uliopita Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa amri ya kuzuia katika dakika ya mwisho kundi la kwanza la wahamiaji na wakimbizi wakiwa kwenye ndege kusafirishwa kuelekea Rwanda.

Kiasi cha watu 27,000 wameingia nchini Uingereza mwaka huu pekee wakati mwaka uliopita kiasi ya watu 46,000 waliingia nchini humo.

Utawala wa Sunak unasema uhamiaji haramu lazima ukomeshwe ili kupunguza shinikizo kwa huduma zinazofadhiliwa na serikali, kama vile afya na makaazi kwa wanaosaka hifadhi.

Je, uhamiaji ni tishio kwa Ujerumani?