1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Sudan yaamuru huduma za Intaneti kurejeshwa

Sylvia Mwehozi
9 Novemba 2021

Mahakama ya Sudan imeamuru kurejeshwa mara moja kwa huduma za mtandao wa intaneti zilizokatwa wakati wa mapinduzi ya kijeshi zaidi ya wiki mbili zilizopita. 

https://p.dw.com/p/42mFA
Sudan | Pro Demokratie Proteste in Khartoum
Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa wakili Abdelazim Hassan aliyezungumza na shirika la habari la AFP, mahakama ya wilaya mjini Khartoum imeamuru huduma za intaneti kurejeshwa mara moja.Kiongozi wa Sudan akutana na ujumbe wa Nchi za Kiarabu

Hata baada ya agizo la mahakama, nchi imesalia bila ya mtandao wa intaneti mapema siku ya Jumanne. Kesi hiyo ilifunguliwa na kundi la wanasheria na jumuiya ya ulinzi wa wateja wa Sudan.

Mahakama pia imeamuru huduma ziendelee kutolewa hata wakati wa mchakato wa rufaa.

Upatikanaji wa intaneti nchini Sudan kwa kiasi kikubwa ulizuiwa tangu Oktoba 25, siku yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyolaaniwa na watu wengi, huku mawasiliano ya simu pia yakitatizika mara kwa mara.

Jenerali mkuu wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan aliivunja serikali, kutangaza hali ya hatari na kuuweka kizuizini uongozi wa kiraia. Waziri Mkuu Abdalla Hamdok alikamatwa na kisha kisha kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani.

Siku moja baada ya mapinduzi Burhan alivishutumu vyombo vya habari vya mtandaoni kwa kuanzisha "uchochezi" lakini pia aliahidi kwamba "huduma za mtandao zitarejea taratibu".

Idadi kubwa ya wanaharakati wanaounga mkono demokrasia wamekamatwa tangu kutokee mapinduzi, ambayo yalisababisha maandamano ya nchi nzima na ukandamizaji uliosababisha vifo vya takriban watu 14, kulingana na madaktari.

Katika hatua nyingine kiongozi wa kijeshi amesisitiza kwamba hana nia ya kuwania nafasi yoyote katika uchaguzi ujao.

Putsch im Sudan | General Abdel Fattah al-Burhan
Kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: /AP/dpa/picture alliance

"Nimesema haya mara kadhaa, ikiwa mambo yataenda kama yalivyopangwa, nitaendelea kufanya kazi hadi uongozi utakapokabidhiwa kwa serikali iliyochaguliwa.  Baada ya hapo, sitakuwa na jukumu la kisiasa. Sitarajii kushiriki kinyang'anyiro chochote cha uchaguzi. Natumai nitaweza kutimiza ahadi hii na kufanya kazi pamoja kama Msudan hadi masuala ya nchi yatakapokabidhiwa kwa serikali iliyochaguliwa."

Wakati huohuo makundi mawili makubwa ya kimataifa ya haki za binadamu yamelitaka jeshi la Sudan kuwaachia maafisa wa serikali, wanaharakati na wengine waliokamatwa wakati wa mapinduzi ya kijeshi.

Katika taarifa ya pamoja mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International pia yametaka kukomeshwa vitendo vya ukamataji holela na ukandamizaji ambao umekuwa ukifanyika kwenye maandamano ya kupinga mapinduzi.

Hii ni mara ya kwanza kwa makundi hayo mawili kutoa taarifa ya pamoja; Awali makundi hayo kila moja lilitoa wito kwa jeshi la Sudan kuwaachia huru viongozi wanaoshikiliwa.

Mnamo Oktoba 25, jeshi la Sudan lilichukua mamlaka na kuvunja serikali ya mpito na kuwakamata watu zaidi ya 100.