1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama muhimu afrika zakutana visiwani Zanzibar

27 Juni 2022

Mahakama tatu muhimu barani Afrika zimekutana visiwani Zanzibar katika kongamano maalum la majadiliano kuhusu ufanisi wa kutoa haki barani humo.

https://p.dw.com/p/4DJge
Wirtschaftsforum in Sansibar
Picha: Salma Said/DW

Mahakama  hizoambazo ni ile ya  Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ) na Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Magharibi (ECOWAS CCJ) miongoni mwa mengine zitazungumzia changamoto walizonazo katika Mahakama hizo na baadae kuzipatiwa ufumbuzi.

Akifungua mkutano huo Rais wa Zanzibar Daktari Hussein Ali Mwinyi alisema bado haki za binaadamu zinaendelea kuvunjwa duniani kote huku akisifia uamuzi wa kufanya mkutano unaozikutanisha taasisi hizo tatu muhimu.

Mkutano huo utafuatiwa na mazungumzo ya pamoja ukiwashirikisha Majaji 30 na Mawakili zaidi ya 50 kutoka Mahakama hizo tatu za bara na kikanda ambapo miongoni mwa mengine utazungumzia mbinu bora za kuimarisha ushirikiano wa kimahakama na utetezi wa haki za binadamu ndani ya bara la Afrika, na utaratibu bora wa utekelezaji wa maamuzi ya mahakama hizo.

Kenia Nairobi Staatshaus Amtseid
Jaji Mkuu wa Nairobi Martha KoomePicha: PPS-presidential press service

Mazungumzo hayo yanatazamiwa kutoa fursa za kubadilishana maarifa na namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazofanana kulingana na Rais wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binaadamu na Watu, Jaji Imani Daud Aboud.

Aidha mkutano huo wa siku tatu unatarajiwa kuwa ni jukwaa la kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama hizo tatu na wadau wengine muhimu, na kubadilishana mawazo juu ya mambo mbalimbali ya msingi yenye maslahi ya pamoja, ikiwa ni pamoja na kanuni bora na taratibu za kukabiliana na masuala yanayojitokeza wakati mahakama hizo zinatekeleza majukumu yao.

Rais wa EACJ Jaji Nestor Kayobera amesema ujumbe waliotoa ni kuomba serikali zote ziheshimu sheria zilizowekwa ili kulinda haki za raia na haki za binaadamu.

Mkutano huo ulitanguliwa na mafunzo ya waandishi wa habari na unafandhiliwa na Taasisi ya haki za binadamu ya Raoul Wallenberg kupitia msaada wa Shirika la Maendeleo la Sweden, na kwa ushirikiano wa Konrad Stiftung, GIZ na Ofisi ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu.