1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kuu Tanzania kuamua kuhusu kesi ya Mbowe

17 Februari 2022

Makahama Kuu nchini Tanzani Ijumaa itatoa uamuzi wake kuhusu kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa chama cha upinzani Chadema, Freeman Mbowe

https://p.dw.com/p/47BGc
Tansania | Prozess gegen Chadema Freeman Mbowe
Picha: Ericky Boniphace/DW

Uamuzi huo kuhusu mashtaka dhidi ya Mbowe pamoja na walinzi wake watatu unatolewa baada ya upande wa mashtaka kukamilisha kutoa ushahidi wake, ikiwaleta mahakamani hapo mashahidi 13, tofauti na awali ilivyohaidi kuwaleta 24. 

Mbowe alikamatwa kwa mara ya kwanza mkoani Mwanza alikokwenda kwa ajili ya kuendesha kongamano lililohusu vuguvugu la madai ya katiba mpya na kisha baadaye alisafirishwa na jeshi la polisi hadi jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuhojiwa kwa siku kadhaa hatimaye alipandishwa kizimbani akishtakiwa kwa makosa ya kuendesha mkakati wa kutekeleza vitendo vya kigaidi ikiwamo kutaka kuchoma moto vituo vya mafuta na kuwazuru baadhi ya viongozi wa serikali.

Tansania John Mnyika Generalsekretär Oppositionspartei CHADEMA
Katibu Mkuu wa Chadema, John MnyikaPicha: DW/Said Khamis

Tangu wakati huo chama chake ikiwamo pia viongozi wa upinzani wamekuwa wakiiokosoa kesi hiyo wakidai ina mkono wa kisiasa. Kumekuwa na kampeni mbalimbali zilizoendelea kutaka Mbowe aachiwe huru na kesi hiyo ifutiliwe mbali kwa madai kuwa kiongozi huyo siyo gaidi.

Katibu wa chama hicho, John Mnyika aliongoza kampeni za kupaza sauti akimsihi Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kuitupia mbali kesi shauri hilo.

Wakati wa kongamano lililowaleta pamoja ofisi ya msajili wa siasa, baadhi ya vyama vya upinzani na Rais Samia, mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia, Zitto Kambwe alimsihi Rais Samia kutumia busara zake kuisitisha kesi hilo.

Kesi hiyo doa kwa taifa

Ombi kama hili limewahi kutolewa mara kadhaa na mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia aliyedai kuwa kesi hiyo kuendelea kuwa mahakamani ni doa kwa taifa na inaleta taswira mbaya katika sura ya kimataifa.

Alivyokutana na Rais Samia, mjini Brussels Ubelgiji, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alitumia fursa hiyo kutaka kesi hiyo ifutwe. Lissu anayeishi ughaibuni tangu aliponusurika katika jaribio la mauaji, alidokeza kuwa Rais Samia aliahidi kulifanyia kazi jambo hilo.

Kesi ya Mbowe mwanasiasa ambaye amekiongoza chama chake cha Chadema kwa zaidi ya miongo miwili imekuwa moja ya mashauri yaliyovuta hisia za wengi ikiwamo wanadiplomasia wa nchi za Magharibu waliokuwa wakibisha hodi mahakamani hapo kila wakati.

Belgien, Brüssel | Samia Suluhu Hassan, Präsidentin von Tansania in Brüssel
Rais Samia Suluhu Hassan na Tundu LissuPicha: Sudi Mnette/Mohammed Khelef/DW

Katika uamuzi wake Ijumaa, mahakama hiyo inatarajia kufanya moja kati ya mambo mawili; mosi kutamka kwamba Mbowe ana kesi ya kujibu na hivyo kufungua milango kwake kuanza kujitetea au kuifutilia mbali.

Wakati wote wa kesi hiyo, wafuasi wa chama chake walifurika mahakamani hapo katika kile kilichoonekana ni hatua ya kumuunga mkono na kumpa matumaini kiongozi wao huyo. Mapema wiki hii upande wa Jamhuri ilikamilisha kuwasilisha mashahidi wake na ingawa hapo awali ilisema ingawaleta mashahidi 24, hadi dakika ya mwisho mashahidi walioletwa ni 13 tu.

Sehemu kubwa ya mashahidi hao walikuwa na maafisa wa polisi ingawa kulikuwa na baadhi waliotoka katika sekta binafsi kama vile kampuni ya simu. Hadi wakati huu bado kuna hisia mseto kuhusi kesi hii na ni kipi mahakama itakiamua.

Kuna uwezekano hali ya ulinzi ikaimarishwa katika eneo la mahakama na viongozi wa Chadema wamewasihi wanachama wake kufurika kwa wingi mahakani hapo kujua hatma ya kiongozi wao.