1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kenya yaidhinisha kutumiwa jeshi kutuliza ghasia

29 Juni 2024

Mahakama nchini Kenya imeidhinisha uamuzi wa kulipeleka jeshi mitaani kuwasaidia polisi, wakati maandamano yakiendelea dhidi ya mswada tata wa kodi ambao serikali imeahidi kuuondoa.

https://p.dw.com/p/4hc6S
Maandamano Kenya
Bunge liliidhinisha jeshi kuwasaidia polisi katika kutuliza ghasia za maandamanoPicha: Brian Inganga/AP/dpa

Wakati magari ya kivita ya kijeshi yalionekana Alhamisi mjini Nairobi, mahakama ilitoa uamuzi jana jioni kuwa hatua ya kutumiwa jeshi iliyoidhinishwa na bunge, ni ya halali kutokana na kuzuka kwa machafuko wakati wa maandamano, ambayo polisi wameshindwa kuyadhibiti. Mahakama ilipinga rufaa iliyowasilishwa na chama cha wanasheria.

Jumanne wiki hii, waandamanaji walivamia bunge na kuchoma moto sehemu ya jengo hilo. Hata hivyo Jaji Lawrence Mugambi pia alionya kuhusu kile alichosema mwenendo hatari ambao huenda ukasababisha nchi kuwa chini ya udhibiti wa jeshi. Kwa hiyo ametaka taarifa sahihi kutoka kwa serikali katika siku mbili kuhusu upeo na muda wa operesheni hiyo.

Soma pia: Blinken akaribisha hatua za rais wa Kenya kutuliza mvutano

Alhamisi kulishuhudiwa maandamano katika maeneo tofauti ya nchi ukiwemo mji mkuu Nairobi. Kulikuwa na ulinzi mkali hasa katika eneo la Ikulu baada ya waandamanaji kusema walipanga kuandamana hadi Ikulu ya Rais.