1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli: Uchaguzi umekwisha, kazi sasa ni kudumisha amani

5 Novemba 2020

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema uchaguzi umekwisha na kazi kubwa iliyo mbele yao ni kudumisha amani, utulivu, kuendelea kuimarisha uhusiano wa kimataifa na kukamilisha miradi ya maendeleo. 

https://p.dw.com/p/3kv00
Tansania Amtseid des Präsidenten John Pombe Magufuli
Picha: Tanzania Presidential Press Service

Rais Magufuli ameitoa kauli hiyo hii leo mjini Dodoma, mara baada ya kula kiapo cha urais cha kulitumikia taifa hilo la Afrika Mashariki kwa kipindi cha miaka mitano kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika hotuba yake, Rais Magufuli amesema kuwa amani na mshikamano vilivyopo nchini Tanzania vinapaswa kudumishwa na kwamba uchaguzi umekwisha na Watanzania wajikite zaidi katika kuchapa kazi hivi sasa kama ilivyo kauli yake tangu aingie madarakani Novemba 5 mwaka 2015.

Aidha, Rais Magufuli ameongeza kusema kuwa anaishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC kwa kuendesha na kusimamia uchaguzi huo uliomalizika kwa amani na utulivu licha ya baadhi ya vyama vya siasa kuonyesha kutoridhika na mchakato mzima wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 28.

Rais Magufuli ala kiapo kuwa rais kwa muhula wa pili Tanzania

Katika sherehe hizo zilizofanyika kwa mara ya kwanza mjini Dodoma tangu kuasisiwa kwa taifa la Tanzania, viongozi wa nchi 20 wakiwemo maraisi kutoka Uganda, Comoro, Zimbabwe pamoja mabalozi 83 wamehudhuria.

Kwa upande wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, akitoa salaam zake za pongezi kwa Rais Magufuli mara baada ya kuapishwa kwake, amesema kuwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki hazina budi kuongeza mshikamano na kutanua masoko ya ndani ili ziweze kujitegemea na kuhakikisha uchumi wa nchi hizo unakuwa.

Rais Magufuli asema uchaguzi umekwisha na sasa ni wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo kulingana na ilani ya chama chake tawala CCM
Rais Magufuli asema uchaguzi umekwisha na sasa ni wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo kulingana na ilani ya chama chake tawala CCMPicha: Tanzania Presidential Press Service

Aidha, Rais Museveni amesema kuwa tatizo la baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika wamegawanyika baada ya kupata uhuru.

Hata hivyo, licha ya kuapishwa kwa Rais Magufuli na makamu wake Samia Suluhu Hassan, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamedai uchaguzi uliomalizika hivi karibuni nchini Tanzania haukuwa huru na haki. Deo Kaji Makomba, DW Dodoma.