1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magharibi wahaha kusaka suluhu ya mzozo wa Ukraine

8 Februari 2022

Ufaransa imesema rais wa Urusi Vladimir Putin ameahidi kutoendeleza shughuli nyingine za kijeshi karibu na Ukraine kwa sasa, ikiwa ni hatua ya awali ya kuhitimisha shughuli hizo kwenye eneo hilo.

https://p.dw.com/p/46fUX
Ukraine-Konflikt - Macron und Putin - PK
Picha: Thibault Camus/Pool AP/dpa/picture alliance

Hatua hii inafuatia mazungumzo kati ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na rais Vladimir Putin wa Urusi. 

Kulingana na maafisa wa Ufaransa ambao hawakutaka kutambulishwa, rais Putin pia amekubali pia kuwaondoa wanajeshi wake wanaofanya luteka katika eneo lililoko nchini Belarus, linalopakana na mipaka ya Ukraine, lakini baada ya luteka hizo kukamilika.

Hata hivyo Putin mwenyewe hakuzungumzia hayo, alipokutana na waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa mazungumzo yake na Macron yaliyochukua masaa sita katika ikulu ya Kremlin mjini Moscow jana Jumatatu, na shirika la habari la Reuters lililochapisha habari hizi pia halikuweza kuthibitisha makubaliano hayo na Urusi.

Soma Zaidi:Nyaraka zavuja, zaonyesha Marekani kutaka kukubaliana na Urusi

Ukraine-Konflikt - Frankreichs Präsident Macron in Moskau - PK
Rais Emmanue Macron ni kiongozi wa ngazi za juu wa kwanza kutoka Ulaya kuzungumza na rais Vladimir Putin wa Urusi kuhusu mzozo wa Ukraine.Picha: Thibault Camus, Pool/AP/picture alliance

Maafisa hao wamesema kwamba kwenye mazungumzo hayo, Macron alikubali kuanzisha majadiliano ya kile walichokiita masuala ya kimkakati, lakini hawakufafanua kwa kina, mazungumzo hayo yatahusisha nini hasa.

Maafisa hao aidha wamesema kulifikiwa makubaliano baina ya wakuu hao ya kufanyika kwa mazungumzo ya kuimarisha juhudi za kidiplomasia ya kusaka suluhu ya mzozo huo kwa mfumo wa Nomandi, ambao Ufaransa na Ujerumani husimama kama waratibu katika mazungumzo yanayohusisha Urusi na Ukraine.

Macron ni kiongozi wa ngazi za juu kabisa wa mataifa ya magharibi kukutana na Putin tangu Moscow ilipoanza kuwapeleka wanajeshi wake karibu na Ukraine, na kuibua hofu inayoelezwa na mataifa hayo kwamba huenda akaivamia.

Marekani na Ujerumani zakubaliana kushirikiana zaidi katika suluhu ya mzozo huo.

Katika hatua nyingine ya muendelezo wa juhudi za kidiplomasia za kusaka suluhu ya mzozo wa Urusi na Ukraine, hapo jana rais Joe Biden wa Marekani amekutana kwa mara ya kwanza na kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, katika ikulu ya White House na kuzungumzia mzozo huo huku rais Biden akisisitiza kwamba iwapo Urusi itaivamia Ukraine watalazimika kuusitisha mradi wa kusafirisha gesi wa Nord Stream 2.

USA Deutschland | Washington | Biden und Scholz bei der Pressekonferenz
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais Joe Biden wa Marekani wakizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo kuhusu mzozo wa Urusi na Ukraine.Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Na hata alipoulizwa ni kwa namna gani watausimamisha mradi huo wa kusafirisha gesi kutoka Urusi hadi Ujerumani, Biden alisema tu kwamba Marekani itaweza kufanya hivyo.

Soma Zaidi: Biden atishia kumwekea Putin vikwazo binafsi

Kansela Scholz, kwa upande wake alizungumzia hatua ya Urusi ya kurundika wanajeshi kwenye mpaka wa Ukraine akisema ni kitisho kikubwa kwa usalama wa Ulaya na ndio maana kuna umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja.

Amesema "Tupo katika wakati mgumu sana na ni vizuri kwamba mimi na Joe tumejadiliana tunachotakiwa kukifanya katika mazingira haya magumu. Ni wazi kuna kitisho cha kijeshi dhidi ya Ukraine, Hatuwezi kubaki kimya. Tunaona idadi ya wanajeshi wa Urusi katika mpaka wa Ukraine. Na hicho ni kitisho kikubwa kwa usalama wa Ulaya. Na ndio maana ni muhimu kuchukua hatua za pamoja, kwamba tunasimama pamoja."

Rais Macron hii leo anatakwenda Ukraine ambapo anatarajiwa kukutana na rais Volodymyr Zelensky, ikiwa ni muendelezo wa juhudi hizi za kidiplomasia za kusaka suluhu.

Mashirika: RTRE/APE