1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini:Matamshi ya Trump yawaacha wachunguzi midomo wazi

Sekione Kitojo
19 Julai 2018

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi  leo(19.07.2018) na matamshi  ya Trump, mjadala kuhusu sera za wakimbizi na watazamaji wa televisheni wanalazimika kulipa fedha kwa ajili ya huduma hiyo.

https://p.dw.com/p/31jyx
Präsidenten von Russland und den Vereinigten Staaten treffen sich in Helsinki
Picha: picture-alliance/dpa/TASS/V. Sharifulin

Mhariri  wa  gazeti la Badische Neueste Nachrichten la mjini  Karlsruhe  anazungumzia  matamshi ya kutatanisha ya  rais  wa  Marekani  Donald Trump katika  vyombo  vya habari. Mhariri  anaandika:

"Kukana  matamshi  yake  pamoja  na  maelezo  ya kichekesho  yamewaacha  wachunguzi  wa  masuala  ya kisiasa  midomo wazi pamoja  na wale ambao wanashindwa kuamini  kilichotokea  wakiduwaa. Si mambo  ambayo  rais wa  Marekani  anaweza  kudai, kwamba  alichosema  watu hawajakielewa. Bila  shaka mtu anapoangalia,  na  kusoma kile  anachosema, ni lazima atambue  kwamba  huyu ni msanii tu. Trump  habadiliki. Na  pia ni  vigumu kumuelewa. Jinsi  anavyochukulia  mambo, inakumbusha  mbinu  jinsi dunia  ya  wafanyabiashara inavyofanya, mchezo wa kuvuruga  masuala  ya  kifedha, ambapo  mashirika yanayofanya  shughuli  za  kifedha  hujaribu  kuvuruga, na kuweka  mbele  maslahi  yake, na  hatimaye  kufikia  lengo lake. Siasa  na  mashirika  ya  kibiashara ni kitu  kimoja, hata  kama  kuna  tofauti  kubwa  ya  utendaji."

Vyombo  vya  habari  vinawawia  vigumu  pia, kuripoti  kwa usahihi  kwa wasomaji  na  wasikilizaji  wa  taarifa, inapokuja  mada  kuhusu mkanganyiko unaotokana  na matamshi  ya  Trump. Anaandika  hivyo  mhariri  wa  gazeti la  Der Neue Tag la  mjini  Weiden. Mhariri  anaadika:

"Waandishi  habari maarufu kama  wa  gazeti  la  Der Spiegel  la  mtandaoni  Sascha Lobo akiandika   makala yake, aliuliza, ni  katika mtazamo  gani  wa  mawazo unaweza  kutenganisha,  na  bila  kuchuja  ujumbe  wa viongozi wafuasi wa  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia. Kutokana  na  kubadilika  kwao, ili  kujiwekea  mpaka baina ya maoni  na  ripoti, ni  kazi  kubwa  mno  hasa  katika vyombo  vya habari halali  vya umma."

Kuhusiana  na  mada  juu  ya  mjadala wa sera za uhamiaji, mhariri  wa  gazeti  la  Stuttgarter Nachrichten anaandika:

"Taifa lenye kifungu cha katiba  kinachozungumzia kuhusu haki isiyopingika  ya  haki  za  binadamu, linapaswa kuchukua  hatua. Hata katika  wakati wa kuwapokea wahamiaji  ambao hawatakiwi, pamoja  na wahamiaji ambao  ni  wahalifu. Ukweli  uko  wazi,  kwamba  nchi  hizi wanakotoka  wahamiaji  hawa  si  nchi  ambazo  hazina sera za  haki  za  binadamu. Lakini  makundi muhimu  ya uchunguzi  wa  haki  za  binadamu  kama  Amnesty International  ama  Human Rights Watch  hawajatoa ushahidi, kwamba ukiukaji  wa  haki  za  binadamu  uko kwa  kiwango  kikubwa ama mfumo  wao hauaminiki  katika nchi  hizi.  Ni  muhimu  kuheshimu  hilo."

Gazeti la  Freie Presse la  mjini  Chemnitz linazungumzia kuhusu  malipo wanayopaswa  kulipa watazamaji wa televisheni hapa Ujerumani. Mhariri  anaandika:

"Pamoja  na uamuzi uliotolewa  jana  na  majaji  wa mahakama  ya  katiba  vituo vya  televisheni  cha  ARD  na ZDF vitakuwa  bado  katika  mbinyo  wa  vyama  vya   siasa kali za  mrengo  wa  kulia na  kizalendo, ambavyo  hutoa kashfa dhidi  yake. Idadi  kubwa  ya  watumiaji  wa  vyombo hivyo  vya  habari, ambao hawatumii vyombo  hivyo, wanaona  ni  kitu cha  kushangaza, kulazimika  kulipa, wakati  hawatazami  kabisa  televisheni  hizo. Majaji  lakini wanasema, hali  itabaki  kama  zamani. Hata  wale  ambao hawana  televisheni, ni  lazima  walipe  malipo  hayo  ya televisheni  na  redio. Hii  si  haki, anaadika  mhariri. Kwa nini  kusiwe  na chombo ambacho kinaweza  kugundua wale  watumiaji  wa  TV kwa  mfano  za  mtandaoni  ama vijana  wanaotumia  kitu  kama  Netflix kwa  mfano  vijana."

 

Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo