1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini: Ziara ya Waziri Heiko Maas nchini Uturuki

Daniel Gakuba
6 Septemba 2018

Wahariri wa Ujerumani leo hii wameandika kuhusu ziara ya Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje nchini Uturuki, muswada wa sheria kuhusu udhibiti wa kodi ya nyumba, na mashambulizi yanayotarajiwa katika mkoa Idlib nchini Syria.

https://p.dw.com/p/34PqB
Türkei Ankara Präsident Erdogan und Heiko Maas Bundesaußenminister, Außenminister, Treffen
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas (kushoto) akipokelewa na Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/AA/M. Kula

Ziara ya Heiko Maas Uturuki, lazima kuukabili ukweli

Tunaanza na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas nchini Uturuki, ambayo ililenga kuboresha uhusiano ulioharibika baina ya nchi hizo mbili. Hatua za kamatakamata zilizoendeshwa na serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa Julai 2016 zilikosolewa vikali na Ujerumani na nchi nyingine za Magharibi. Raia wa Ujerumani ni miongoni mwa waliokamatwa na kutiwa jela kwa tuhuma za kuunga mkono wapinzani wa serikali ya mjini Ankara.

Likiandika kuhusu ziara ya waziri Maas, gazeti la Rhein-Zeitung la mjini Koblenz limesema waziri huyo hana budi kuukabili ukweli bila kuupita pembeni. Mhariri wa gazeti hilo anasema raia wa Ujerumani wako jela nchini Uturuki, kwa sehemu kubwa bila mashitaka yanayoeleweka, mbali na kushukiwa kuwa washirika wa maadui wa Rais Erdogan. ''Waziri Heiko Maas anabidi kuyakabili matatizo hayo, kwa sababu hata kwa nchi mwanachama wa Umoja wa Kujihami - NATO, uhuru wa watu kukusanyika, uhuru wa kutoa mawazo, na haki za binadamu, ni masuala yasiopaswa kujadiliwa.

Erdogan, mshirika wa maslahi wa Ulaya

Katika suala hilo hilo la uhusiano baina ya Uturuki na nchi za Magharibi, gazeti la Weser-Kurier la mjini Bremen limesema katika uhariri wake, kwamba vikwazo vya Marekani vimemweka Rais Erdogan katika hali dhaifu, ambayo imemlazimisha kumeza dawa chungu ya kuujongelea Umoja wa Ulaya ambao kawaida haupendi. Kwa upande mwingine lakini, gazeti hilo linaandika, Umoja wa Ulaya nao unajikuta katika hali tete kiusalama, na kwa hivyo wenyewe pia hauna chagua mbadala, zaidi ya kuukubali mkono wa mtawala huyo wa kiimla, ambaye ana ufunguo wa kuihakikishia Ulaya usalama kwenye mpaka wake wa Kusini.

Mashambulizi dhidi ya Idlib, Assad hatapata ushindi wa kudumu

Gazeti la Landeszeitung la mjini Lüneburg linazungumzia wingu la mashambulizi linaougubika mkoa wa Idlib Kaskazini Magharibi mwa Syria, ambao unabakia chini ya udhibiti wa waasi. Gazeti hilo linasema muda unasogea haraka na hakuna uwezekano mkubwa wa kumshawishi Rais Bashar al-Assad asifanye mashambulizi dhidi ya mkoa huo.

Linasema baada ya kuuchukua mji wa Aleppo kufuatia mzingiro wa muda mrefu uliosababisha njaa kubwa kwa wakazi wake, na mashambulizi makali yaliyowafurusha waasi kutoka Ghouta Mashariki, ni zamu sasa ya Idlib kuangukia katika umwagaji damu. ''Hata hivyo'', Landeszeitung linaonya, ''ushindi wa kimabavu wa Assad sio wa kudumu, kwa sababu endapo majeshi ya Urusi yataondoa msaada wao wa angani, na wapiganaji wa Iran wakarudi makwao, Assad atajikuta tena chini ya shinikizo, kwa sababu chuki dhidi yake miongoni mwa wananchi haina kipimo''.

Muswada wa kudhibiti kupanda kwa kodi ya nyumba, turufu ya kisiasa

Mada nyingine iliyoangaziwa na magazeti ya Ujerumani katika uhariri wake wa leo, ni kupitishwa kwa muswada wa udhibiti katika ongezeko la nyumba hususan katika miji mikubwa. Magazeti mengi yameukaribishwa kwa tahadhari muswada huo uliopitishwa na baraza la mawaziri la shirikisho jana Jumatano (05.09.2018). Berliner Zeitung limesema, '' Bila shaka muswada huo unaleta ahueni kwa wapangaji, lakini sio suluhisho la kushangiliwa.'' Sababu, linasema gazeti hilo, ni kwamba kupitishwa kwake kumetokana na muafaka kati ya vyama vikuu vinavyounda serikali ya mseto, CDU/CSU na SPD, ambavyo kwavyo, kufanikisha malengo ya kisiasa ni bora kuliko suluhisho endelevu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman