Maelfu ya watu waandamana Niger kupinga vikwazo vya ECOWAS
3 Agosti 2023Maandamano hayo yaliyoitishwa na utawala wa kijeshi pamoja na mashirika ya kiraia katika siku hii ambayo Niger inasherehekea siku ya uhuru wake, yaliitikiwa na maelfu ya watu ambao baadhi walikuwa na bendera za Niger na Urusi.
Maelfu ya watu walisikika wakiimba kwa kuunga mkono nchi jirani ambazo pia miaka ya hivi karibuni zimeshuhudia mapinduzi ya kijeshi huku wakitoa kauli za kashfa kwa Ufaransa na mataifa ya Magharibi wakitaka kuondoka mara moja kwa vikosi vya mataifa hayo.
Soma pia: Utawala wa kijeshi waitisha maandamano makubwa Niger
Waandamanaji hao walikemea pia hatua ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ambayo imeiwekea Niger vikwazo kadhaa vya kiuchumi na kusema inaweza kuidhinisha matumizi ya nguvu ikiwa kufikia Jumapili hii, utawala wa kijeshi hautomrejesha Bazoum madarakani.
Senegal imetangaza hii leo kuwa itawatuma wanajeshi wake Niger ikiwa ECOWAS itaamua kutuma kikosi nchini humo. Jenerali Abdourahamane Tiani aliyejitangaza kuwa mkuu wa nchi baada ya mapinduzi yaliyomuondowa madarakani rais Mohamed Bazoum, amesema vikosi vya nchi hiyo viko imara.
" Hapana, kamwe vikosi vya ulinzi vya Niger havitogawanyika na kuzozana kati yao kwa sababu za kisiasa zisizo na maana. Vikosi vyetu vya ulinzi na usalama ndio nguzo ya umoja wa kitaifa nchini Niger. Ni kwa pamoja ndipo tutakabiliana na adui katika uwanja wa mapambano na mara nyingi kwa kujitolea mhanga."
Wasiwasi wa mataifa ya Magharibi
Ubalozi wa Ufaransa huko Niamey umewahimiza watawala wa Niger kuchukua hatua zote kuhakikisha usalama na ulinzi wa ofisi na wafanyakazi wa kidiplomasia nchini humo.
Soma pia: Ujumbe wa ECOWAS wawasili Niger
Serikali ya Ufaransa imesema Alhamisi kuwa imewahamisha watu 1,079 kutoka Niger wakati operesheni yake ikikamilika katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi iliyokumbwa na mapinduzi.
Ufaransa yenye jumla ya wanajeshi 1,500 nchini Niger, kwa ushirikiano na mataifa mengine ya Ulaya na Marekani, imekuwa ikiendesha operesheni za pamoja za kupambana na makundi ya kigaidi ya al-Qaida na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS.
Utawala mpya wa kijeshi nchini Niger haujaweka wazi ikiwa unakusudia kushirikiana na Moscow au kushikamana na washirika wake wa Magharibi lakini swali hilo limekuwa kiini cha mzozo wa kisiasa unaoendelea. Nchi jirani za Mali na Burkina Faso ambazo zote zinatawaliwa kijeshi zimegeigeukia Urusi.
Niger inachukuliwa kama mshirika wa mwisho wa kutegemewa wa nchi za Magharibi katika ukanda wa Sahel lakini baadhi ya watu eneo hilo wanaiona Urusi na kundi lake la mamluki la Wagner kama washirika mbadala na wakuaminika.