1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wapiganaji waelezwa kuunga mkono Hezbollah

23 Juni 2024

Maelfu ya wapiganaji kutoka makundi yanayoungwa mkono na Iran Mashariki ya Kati wako tayari kwenda Lebanon kuungana na Hezbollah katika vita vyake na Israel ikiwa ni mzozo unaoendelea kutanuka na kuwa vita kamili.

https://p.dw.com/p/4hOns
Lebanon | Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah
Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah akitoa hotuba katika kumbukumbu ya Kamanda Mkuu Taleb Sami Abdallah.Picha: EPA/WAEL HAMZEH

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa maafisa wa Iran na wachambuzi. Hali katika eneo la mpakani la kaskazini imezidi kuwa mbaya kwa mwezi huu baada ya shambulizi la Israel kumuua kamanda mwandamizi wa Hezbollah, huko kusini mwa Lebanon.

Kufuatia kitendo hicho Hezbollah ililipiza kisasi kwa kurusha mamia ya roketi na ndegezisizo na rubani za kulipuka katika ardhi ya Israel kwa upande wa  kaskazini.

Majibizano ya mashambulizi ya takribani kila siku yanatokea katika mpaka wa kaskazini wa Lebanon na Israel tangu kundi la Hamas lifanye shambulio la umwagaji damu kusini mwa Israel mapema Oktoba ambalo lilizusha vita huko Gaza.