1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yanafanyika sehemu mbali mbali Ulimwenguni

Faiz Musa 15 Machi 2019

Maelfu ya wanafunzi wamesusia masomo na kushiriki maandamano ya kuwashinikiza viongozi kuchukua hatua juu ya mabadiliko ya tabia nchi barani Ulaya na katika mabara mbalimbali kote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/3F6xW
Fridays for future Schüler Schülerinnen Streik Schulstreik Klima Klimawandel Hongkong
Picha: AFP/Getty Images/A. Wallace

Wanafunzi walitoka madarasani katika taifa la Australia na New Zealand na kuingia katika mwa miji mikuu ya nchi hiyo wakiandamana huku wakiwa wamebeba mabango yanayotoa ujumbe wa kuwasuta viongozi na kuwaeleza iwapo hawatachukua hatua kama watu wazima basi wao watoto watachukua hatua.

Maandamano hayo pia yaliwavutia maelfu ya watu waliojiunga nayo wakisema iwapo hatua hazitochukuliwa kuzuia gesi chafu inayotoka viwandani basi kila mmoja ataathirika. Maandamano makubwa zaidi yalifanyika Ulaya na Marekani.

Mmoja wa wanafunzi mjini Sydney Callum Frith akiwa katika maandamano hayo aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba kama wanafunzi na vijana wameamau kutumia njia hiyo kuonyesha uwezo walionao katika kufanya maamuzi ya busara.

Fridays for future Schüler Schülerinnen Streik Schulstreik Klima Klimawandel Seoul
Wanafunzi wakishiriki maandamano ya mazingira mjini Seoul, Korea Kazkazini.Picha: Getty Images/Chung Sung-Jun

Naye mwanafunzi wa umri wa miaka 14 kutoka New Zealand alisema serikali inahitajika kufanya mabadiliko na ndio maana wameandamana siku ya masomo ili kuipa ujumbe mzito kuhusu hali inayoendelea kuwa mbaya ya mazingira.

Baadhi ya viongozi Ulimwenguni wawaunga mkono wanafunzi.

Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Arden aliunga mkono mgomo wa wanafunzi hao na vilevile kuahidi kutenga dola milioni 68 kwa ajili ya kupunguza gesi chafu inayotoka viwandani.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron pia waliunga mkono maandamano hayo.

Waziri wa Elimu wa Australia, Dan Tehan aliyapinga maandamano hayo na kusema iwapo wanafunzi wanaona jambo hilo ni muhimu wangelifanya siku ambazo sio za masomo.

Fridays for future Schüler Schülerinnen Streik Schulstreik Klima Klimawandel Sydney
Mmoja wa waandamanaji akiwa na bango mjini Sydney, Australia.Picha: Getty Images/J. Gourley

Wanasayansi wanasema uchomaji wa nishati ya makaa ya mawe unasababisha gesi chafu ambayo inachangia kuongezeka kwa viwango vya joto ulimwenguni, hivyo kuleta mafuriko, ukame na kuongezeka kwa viwango vya maji baharini.

Katika kongamano la kimataifa kuhusu mazingira lililofanyika mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015 mataifa yaliweka ahadi ya kuchukua hatua za kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya makaa ya mawe ili kupunguza kiwango cha joto kwa nyuzijoto mbili.

Kulingana na jopo la wanasayansi wa Umoja wa Mataifa, hali ya joto inazidi kuongezeka kote ulimwenguni, huku ripoti ya mwaka 2017 ikionyesha kwamba gesi chafu ya Carbon Dioxide imezidi.

(APE/RTRE)