1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya Wakenya wajitokeza kupiga kura

9 Agosti 2022

Maelfu ya Wakenya wamefika vituoni kupiga kura kumchagua rais wa tano wa nchi hiyo. Ulinzi umeimarishwa kote nchini huku maafisa 150,000 wakipiga doria kuzuwia uwezekano wowote wa machafuko.

https://p.dw.com/p/4FJEQ
Kenia Kibera Slum Nairobi Wahlen
Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Wakenya waliraukia vituo vya kupiga kura alfajiri ili kuweza kutimiza haki yao ya kikatiba. Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa 12 asubuhi hii. Baadhi vilipata misukosuko ya kiufundi ila kwa kiasi kikubwa operesheni inaendelea vizuri.

Vituo 46,000 vimeteuliwa kuwawezesha Wakenya waliojiandikisha kupiga kura.

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto anayewania urais kupitia chama cha UDA na Muungano wa Kenya Kwanza aliwasili kwenye Shule ya Msingi ya Kosachei iliyoko kwenye ngome yake ya Sugoi akisindikizwa na mkewe Rachel Ruto.

Mgombea wa urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga alipokelewa kwa vifijo na nderemo alipowasili kwenye kituo cha Shule ya Msingi ya Old Kibera kupiga kura akisindikizwa na mkewe Ida Odinga.

Kenia Wahlen Raila Odinga William Ruto
Wagombea urais wakuu wa Kenya, William Ruto na Raila OdingaPicha: AFP

Mgombea mwenza wa urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja, Martha Karua amewarai Wakenya kushiriki kwenye uchaguzi alipopiga kura kwenye kituo cha Shule ya Msingi ya Mugumo iliyoko kwenye kaunti ya Kirinyaga.

Katika kaunti ya Kiambu eneo la Gatundu Kusini, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alipiga kura kwenye Shule ya Msingi ya Mutomo kama raia wa kawaida na wala sio mgombea kama ilivyokuwa mwaka 2013 na 2017.

Kwa upande mwengine, mgombea wa urais wa chama cha Roots George Wajackoyah alishindwa kupiga kura kwenye eneo la Matungu baada ya mashine za kiems za kuwatambua wapiga kura kidijitali kupata hitilafu. Vituo vya kupigia kura vitafungwa Jumanne jioni.