1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya raia wakimbia mashambulizi Idlib

23 Desemba 2019

Maelfu ya raia wamekimbia vita katika mkoa wa Idlib nchini Syria. Rais wa Uturuki Recep Erdogan ameonya kuhusu wimbi jipya la wahamiaji na kwamba zaidi ya wahamiaji 80,000 wanakimbia eneo hilo kuelekea mpaka wa Uturuki.

https://p.dw.com/p/3VFWu
Syrien, Idlib: Erneute Zerstörung und Flucht
Picha: Getty Images/AFP/A. Watad

Vikosi vya serikali nchini Syria vimeikamata miji na vijiji kadhaa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo kutoka mikononi mwa wanamgambo, baada ya makabiliano, na kusababisha maelfu ya raia kukimbia. Hayo yamejiri huku rais wa Uturuki akionya kuwa takriban wahamiaji 80,000 wanayakimbia makwao Syria katika wimbi jipya la uhamiaji. 

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alionya hapo jana kuwa nchi yake haitashughulikia peke yake wimbi jipya la wahamiaji wa Syria wanaokimbia mashambulizi kaskazini magharibi mwa mkoa wa Idlib.

Maelfu kwa maelfu ya Wasyria wameyakimbia makaazi yao kuelekea mpaka wa Uturuki tangu Disemba 16 wakati mashambulizi makali yalipoanza ene la Maaret al-Numan. Rais Erdogan ambaye amekuwa akiutuhumu Umoja wa Ulaya kwa kutotoa msaada wa kutosha kifedha kusaidia wahamiaji, amezionya nchi za umoja huo kuwa wimbi jipya la wahamiaji litawaathiri.

"Zaidi ya ndugu zetu 80,000 kutoka Idlib wameanza kukimbia mabomu huko na wanaenda katika mipaka yetu. Ikiwa machafuko dhidi ya watu wa Idlib hayatakoma, idadi hii itaongezeka mara saba. Katika hali hiyo, Uturuki hautabeba peke yake mzigo wa wahamiaji. Nchi zote za Ulaya zitahisi athari hasi ya hali hiyo hasa Ugiriki.” Amesema Erdogan.

Juhudi za kuukamata mji wa Maaret al-Numan

Mkoa wa Idlib ambao una wanamgambo wengi, pia na wakaazi milioni tatu, wakiwemo wakimbizi wa vita kutoka maeneo mengine ya Syria. Utawala wa nchi hiyo umeapa mara kwa mara kuwa utachukua udhibiti wa mkoa huo.

Sehemu ambayo imeharibiwa na mashambulizi katika mji wa Maaret al-Numan nchini Syria.
Sehemu ambayo imeharibiwa na mashambulizi katika mji wa Maaret al-Numan nchini Syria.Picha: Getty Images/AFP/A. Ketaz

Shirika la haki za binadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza limeripoti kuwa, vikosi hivyo vya serikali pamoja na washirika wake vimekamata maeneo hayo ya mkoa wa Idlib, mnamo wakati ndege za kivita za Urusi ziliendelea kufanya mashambulizi kusini mwa mkoa huo na kuua raia tisa waliokuwa wakijaribu kukimbia eneo hilo linaloshambuliwa.

Mashambulizi ya ardhini yanayofanywa na vikosi vitiifu kwa rais wa Syria Bashar al-Assad, vimeusogeza utawala huo kukaribia kukikamata kituo kikubwa zaidi cha mjini kilichosalia cha ngome ya upinzani.

Mkuu wa shirika la haki za binadamu Rami Abdul Rahman ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mashambulizi ya hivi karibuni ni juhudi za kusogea karibu eneo la Maaret al-Numan.

Wakaazi wa kusini mwa Idlib wameyakimbia makaazi yao kwa kuhofia mashambulio zaidi.

Kulingana na shirika la haki za binadamu linalofuatilia vita n chini Syra, zaidi ya watu 30,000 wamekimbia kusini mwa Idlib katika siku za hivi karibuni, na zaidi ya raia 40 wameripotiwa kuuawa wiki iliyopita.

Vyanzo: AFPE, ADPAE