1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakimbilia Mogadishu kutokana na ukame, njaa

28 Februari 2022

Wiki hii Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa lilionya kuwa watu milioni 13 katika eneo hilo, zikiwemo sehemu za Ethiopia na Kenya, watakabiliwa na njaa kali katika robo ya kwanza ya 2022

https://p.dw.com/p/47jMz
Hunger in Somalia
Picha: picture alliance/AP Photo/F. A. Warsameh

Wakiwa wameketi chini ya jua kali, wanawake na watoto wenye njaa wanasubiri msaada wa chakula katika kambi nje kidogo ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu

Wanasema wametembea kwa siku kadhaa, wakikimbia ukame ambao sasa umeharibu sehemu kubwa ya vijiji vya Somalia.

Takwimu zinatarajiwa kuongezeka zaidi, katika miezi kadhaa ijayo, huku eneo la Pembe ya Afrika likikabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP,  limesema msaada wa haraka unahitajika ili kuepusha janga kubwa la kibinaadamu.

Pembe ya Afrika kwa muda mrefu imekuwa katika hatari ya ukame na njaa, hali inayochochewa na vurugu za kutumia silaha.

Dürre in Somali Region
Mifugo wameangamia kutokana na ukame SomaliaPicha: Mulugeta Ayene/UNICEF/AP/picture alliance

Serikali ya Somalia mwezi Novemba ilitangaza hali ya dharura ya kibinaadamu kutokana na ukame, huku sehemu zilizoathirika zaidi zikiwa ni  maeneo ya kusini na kati ya Jubba ya Chini, Geddo na mikoa ya Shabelle ya Chini.

Utafiti uliofanyika  mwezi Novemba ulihusisha mikoa 15 kati ya 18 ya Somalia na ulibaini kuwa familia nyingi zilikuwa zikikosa mlo wa mara kwa mara.

Nchini Somalia, watu 250,000 walifariki  kutokana na njaa mwaka 2011, wakati Umoja wa Mataifa ukitangaza baa la njaa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na nusu yao walikuwa watoto.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, limesema linahitaji dola milioni 327 kushughulikia mara moja mahitaji ya watu milioni 4.5 katika muda wa miezi sita ijayo, ikiwa ni pamoja na Somalia.

Kikosi kazi kimeundwa mapema mwezi huu na Waziri Mkuu Mohamed Roble hukusanya na kusambaza michango kutoka kwa jumuiya ya wafanyabiashara pamoja na Wasomali walioko ughaibuni.

Mmoja wa wanawake waliokusanyika kupata msaada wa chakula, Faduma Ali, anasema ametembea zaidi ya kilomita 500 kutoka nyumbani kwake huko Saakow, mji katika jimbo la Jubba ya Kati, hadi Mogadishu.

Ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba matatizo yanayomkabili  yote yanatokana na ukame akiongeza na hapa namnukuu: "Hatukuwa na maji na mifugo yetu imeangamia na nimepopoteza kila kitu, nimetembea barabarani kwa siku saba."

APE