1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Maelfu wajitokeza kuonyesha mshikamano na wahamiaji

8 Agosti 2024

Maelfu ya waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi wameingia barabarani katika miji mbalimbali nchini Uingereza kupinga vurugu zilizochochewa na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.

https://p.dw.com/p/4jF29
Waandamanaji wapinga chuki dhidi ya wahamiaji mjini London, Uingereza
Waandamanaji wapinga chuki dhidi ya wahamiaji mjini London, UingerezaPicha: Burak Bir/Anadolu/picture alliance

Meya wa jiji la London Sadiq Khan amewashukuru watu waliojitokeza kuonyesha mshikamano dhidi ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya uislamu. 

Polisi wamekuwa katika hali ya tahadhari katika maeneo kadhaa nchini Uingereza kukabiliana na matukio ya vurugu – lakini kama ilivyo katika sehemu kubwa ya nchi hiyo – maandamano ya amani yalifanyika kama ishara ya kuonyesha mshikamano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Jana jioni, waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi na ufashisti walijitokeza kwa maelfu katika miji ya London, Birmingham, Bristol na Newcastle.

Soma pia: Polisi Uingereza iko tayari kukabiliana na vurugu za waandamanaji

Waandamanaji hao waliimba na kubeba mabango yaliyosema, "zuia siasa kali za mrengo wa kulia.”

Huyu ni mmoja wa waliojitokeza kuonyesha upendo kwa wageni.

"Kwa kweli, nimeona ishara ya umoja. Ninaona watu wakikusanyika kuonyesha umoja kama methali inavyosema, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu."

Polisi washika doria katika maeneo mbalimbali Uingereza

Maandamano ya kuunga mkono wageni yafanyika Walthamstow
Maandamano ya kuunga mkono wageni yafanyika WalthamstowPicha: Aysu Bicer/Anadolu/picture alliance

Kupitia mtandao wa kijamii wa X, meya wa London Sadiq Khan ametoa shukrani kwa polisi wa mji mkuu huo kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuimarisha usalama. Takriban maafisa wa polisi 1,300 walitumwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo ili kushika doria.

Matukio ya vurugu yaliyohusisha uvamizi dhidi ya misikiti na sehemu wanamolala wahamiaji yalishuhudiwa katika miji kadhaa ya England na Ireland Kaskazini na ambayo yalichochewa na taarifa za upotoshaji kuhusu mauaji ya watoto watatu mnamo Julai 29.

Soma pia: Starmer kuunda 'jeshi la dharura' kukabiliana na vurugu

Naibu kamishna wa polisi Andy Valentine pia ametoa shukrani kwa watu waliojitokeza kuonyesha mshikamano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Kwa mujibu wa polisi, waandamanaji mjini Sheffield waliimba kwa sauti kubwa, "wakimbizi wanakaribishwa hapa” wakati miji ya Birmingham na Brighton maelfu ya wengine pia walijitokeza kuwaunga mkono wageni.

"Nilihisi umuhimu wa kuja hapa ili kuwalinda wageni. Kumekuwa na hofu juu ya kinachoweza kutokea na niliona ni muhimu sana kujitokeza, niko hapa kuilinda jamii yetu.”

Watu 400 wamekamatwa kwa kuhusika na vurugu

Serikali ya Uingereza ilikuwa imeweka polisi 6,000 wa kutuliza ghasia katika hali ya tahadhari baada ya kutolewa tangazo na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia juu ya nia ya kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Polisi wakikabiliana na waandamanaji wa siasa kali za mrengo wa kulia mjini Bristol
Polisi wakikabiliana na waandamanaji wa siasa kali za mrengo wa kulia mjini BristolPicha: JUSTIN TALLIS/AFP

Waziri wa mambo ya ndani Yvette Cooper amewashukuru maafisa wote wa polisi kwa kujitolea kwao kuhakikisha usalama.

Waziri Mkuu Keir Starmer, mwendesha mashtaka mkuu wa zamani ambaye anakabiliwa na mgogoro wa mapema baada ya kushinda katika uchaguzi wa Julai 4, amewaonya wote wanaochochea vurugu kwamba chuma chao ki motoni.

Soma pia: Waziri Mkuu Starmer aapa kuwawajibisha walioshiriki ghasia

Msimamo huo mkali wa serikali kwa namna fulani umeonekana kuwatisha baadhi ya watu waliokuwa na nia ya kufanya vurugu.

Katika muda wa zaidi ya wiki moja, tayari watu 400 wamekamatwa, ikiwemo kifungo cha miaka mitatu kwa mwanamume mmoja aliyetambulika kama Derek Drummond, mwenye umri wa miaka 58, aliyemshambulia polisi.