1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana kulaani dhulma dhidi ya wanawake

26 Novemba 2023

Maelfu ya watu waliandamana kote duniani hapo jana Jumamosi kulaani ukatili dhidi ya wanawake katika siku ya kimataifa inayolenga kutokomeza uhalifu huo.

https://p.dw.com/p/4ZS99
Italia| Roma| Maandamano
Maelfu ya waandamanaji mjini Roma kulaani ukatili dhidi ya wanawake Picha: Alessandra Tarantino/AP Photo/picture alliance

Maelfu ya watu waliandamana kote duniani hapo jana Jumamosi kulaani ukatili dhidi ya wanawake katika siku ya kimataifa inayolenga kutokomeza uhalifu huo.

Katika taarifa yake, Rais wa Marekani Joe Biden, alisema kuwa janga la ukatili wa kijinsia linaendelea kuleta maumivu na dhuluma kwa wengi.

Italia, ambayo imetikiswa na mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 22 anayedaiwa kuuawa na mpenzi wake wa zamani, takriban watu 50,000, walifanya maandamano huko Roma, ambapo ukumbi wa Colosseum ulipaswa kuwashwa mataa ya rangi nyekundu baadaye hapo jana Jumamosi. Haya ni kulingana na shirika la habari la AGI.

Nchini Uturuki, wanawake wapatao 500 walikusanyika katika eneo la Sisli huko Istanbul, wakishika mabango yaliyosomeka, ''hatutanyamaza na wanawake wameungana na kupinga unyanyasaji unaofanywa na wanaume''. Maandamano pia yalifanyika mjini Ankara.

Soma: Kampeni ya siku 16 kupinga ukatili dhidi ya wanawake Burundi

Nchini Ufaransa, maelfu ya watu wakiwa wamevalia rangi ya zambarau, inayowakilisha harakati za usawa wa kijinsia, walizunguka katika mitaa ya Paris na miji mingine wakiwa na ujumbe wa kupinga visa vya ubakaji na hatua za kuwalinda wasichana pamoja na kumwelimisha mtoto wa kiume.