1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana kudai udhibiti wa silaha Marekani

25 Machi 2018

Katika ongezeko la kihistoria la uhamasishaji wa vijana kisiasa, maelfu ya vijana na wanaowaunga mkono wameandamana Marekani kote kudai udhibiti mkali wa silaha nchini humo, wakiapa kutumia nguvu ya kura kutimiza lengo.

https://p.dw.com/p/2uvmp
Washington  March For Our Lives Protestmarsch
Picha: Getty Images/A. Wong

Waliingia katika mitaa ya mji mkuu wa taifa hilo na miji mingine kama Boston, New York, Chicago, Houston, Minneapolis, Phoenix, Los Angeles na Oakland, California, katika idadi ambayo ilionekana wakati wa enzi za Vita vya Vietnam, na kuwazoa wanaharakati ambao kwa muda mrefu wamevunjwa moyo na mkwamo katika mjadala wa umiliki wa silaha na kuzijumuisha sauti nyingi mpya za vijana.

Walihamasishwa na viongozi wapya kabisaa: Wanafunzi manusura wa shambulio la shule mjini Parkland, Florida ambalo liligharimu maisha ya watu 17 Februari 4. "Ukisikiliza kwa karibu zaidi, unaweza kusikia watu walioko madarakani wakitetemeka," alisema manusura wa Parkland David Hogg mbele ya umati wa waandamanaji waliofurika mtaa wa Pennsylvania mita chache kutoka majengo ya bunge na karibu na ikulu ya White House.

"Tunalipeleka hili kwenye uchaguzi, kwa kila jimbo na kila mji. Tutahakikisha watu bora zaidi wanaingia na kugombea katika uchaguzi wetu, siyo kama wanasiasa lakini kama Wamarekani." Kwa sababu hii," alisema akinyoosha kidole nyuma yake kwa kuba la jengo la bunge, " hii haiwezi kukata shauri hilo."

USA Washington March for our Lives - Jaclyn Corin und Yolanda Renee King
Yolanda Renee King, mjukuu wa Martin Luther King Jr., kushoto, akisindikizwa na Jaclyn Corin, mwanfunzi wa shule ya Marjory Stoneman Douglas mjini Parkland, Florida, na mmoja wa waandaji wa maandamano, akizungumza wakati wa maandamano hayo yaliopewa jina la "Matembezi ya Maisha Yetu."Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Washiriki hadi miaka 9

Baadhi ya sauti za vijana zilikuwa ndogo sana. Yolanda Renee King, mjukuu wa Martin Luther King Jr. mwenye umri wa miaka 9, alinukuu kutoka maneno maarufu ya kiongozi huyo wa haki za kiraia katika kutangaza jukwaani: "Nina ndoto kwamba inatosha. Kwamba huu unapaswa kuwa ulimwengu ulio huru na silaha."

Kwa muonekano wote - hakukuwa na tarakimu rasmi - Mkutano wa Matembezi ya Miasha Yetu mjini Washington ulishindana na maandamano ya wanawake mwaka uliopita ambayo yalihudhuriwa na watu wengi zaidi kuliko idadi iliokuwa imetabiriwa ya 300,000.

Chama cha Wamiliki wa bunduki kilikuwa kimya kwenye ukurasa wake wa Twitter wakati maandamano hayo yakianza, ikilinganishwa na Machi 14, kilipochapisha picha ya bunduki ya mashambulizi na ujumbe usemao, "nitadhibiti bunduki zangu mwenyewe, ahsante."

Msemaji wa Trump aeleza juhudi za utawala

Rais Donald Trump alikuwa jimboni Florida kwa mapumziko ya mwishoni mwa wiki na pia hakuandika chochote kwenye twitter.

Msemaji wa ikulu ya White House Zach Parkinson alisema: "Tunawapongeza vijana wengi wa Kimarekani wanaotekeleza haki zao za Mabadiliko ya kwanza ya katiba ya Marekani leo." Alibainisha juhudi za Trump kupiga marufuku vifaa vinavyoongeza ufanisi wa bunduki za kiraia, na uungaji wake wa hatua za kiusalama kwa shule pamoja na uchunguzi wa ziada kwa wanaoununua silaha.

Tangu tukio la Florida, wanafunzi wamejiunga na wimbi la kudai udhibiti wa silaha ambalo limekuwa likiendelea kwa miaka kadhaa - ambalo hata hivyo linakabiliana na hasimu mwenye nguvu kubwa - NRA, mamilioni ya waungaji wake mkono na wabunge waliopinga kuguswa kwa namna yoyote ile haki zao za kumiliki silaha.

USA Washington "March for Our Lives"
Watu wakiangalia kutokea roshani ya jengo la Makumbusho wakati wanafunzi na wanaharakati wa udhibiti wa silaha wakiandamana mjini Washington, Marekani, Machi 24, 2018.Picha: Reuters/L. Millis

Matumaini ya mabadiliko

Waandaji wanatumaini kuwa idadi kubwa ya washiriki wa maandamano hayo na wazungumzaji wengi wenye umri wa chini ya miaka 18, vitasababisha mabadiliko, kuanzia na uchaguzi wa kati ya muhula wa Bunge baadae mwaka huu. Katika muktadha huo, sauti za "Waondoeni" zilihanikiza katika makundi yaliokusanyika mjini Washington.

Emma Gonzalez, mmoja wa wanafunzi wa kwanza wa shule ya sekondari ya Marjoy Stoneman Douglas ya mjini Florida kuanza kuzungumza baada ya shambulio, aliwahimiza waliofikisha umri wa kupiga kura kujitokeza kwa wingi na kupiga kura. Katika hotuba yake, alitaja majina ya wahanga wa Parkland, na kisha akaongoza kimya cha dakika sita, muda ambao mshambuliaji alitumia kuwauwa.

"Tutaendelea kuwapigania marafiki zetu waliokufa," alisema Delaney Tarr, manusura mwingine wa Parkland. Washiriki walinguruma wakikubaliana na tamko lake alipobainisha takwa kuu la wanafunzi: marufuku dhidi ya silaha za kivita kwa watu wote kasoro wapiganaji..

Wanafunzi waandamanaji walitoa wito wa kupigwa maruku matumizi ya magazini zenye uwezo mkubwa na silaha za mashambulizi kama iliyotumiwa na mshambuliaji wa Parkland, ukaguzi wa kina wa historia za wananuzi wa silaha, na kupandisha umri wa chini kabisaa kwa mtu kununua silaha.

Frankreich March For Our Lives Paris
Maandamano ya mshikamano mjini Paris, Ufaransa kuwataka wanasiasa wa Marekani kubadilisha sheria za silaha nchini humo.Picha: picture-alliance/MAXPPP/Wostok Press/N. Joubert

'Hatuhitaji waalimu wenye silaha'

Wito wa rais wa kuwapatia silaha baadhi ya walimu ulipingwa vikali, na kutoka kwa wakosoaji wenye umri mdogo kama Zoe Tate wa miaka 11 kutoka Gaithersburg, Maryland.

"Nadhani bunduki ni bubu. Inatisha vya kutosha kwa walinzi tulio nao mashuleni," alisema. "Hatuhitaji walimu waliobeba silaha sasa. Inanishangaza kuona kuwa nahitaji kufafanua jambo hilo kwa watu wazima."

Mjini Parkland kwenyewe kulifanyika maandamano yaliohudhuriwa na watu zaidi ya 20,000 waliokusanyika kwenye bustani karibu na shule ya Florida, wakitoa kaulimbiu kama vile "Inatosha" na wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe unaosomeka "kwanini bunduki zenu zinapewa kipaumbele kuliko maisha yetu?" na "Kura zetu zitakomesha risasi."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Jacob Safari