Madrid yaiduwaza Bayern na kutinga fainali
9 Mei 2024Kwa muda ilionekana kana kwamba Bayern Munich wataishinda mechi hiyo na kufuzu fainali, ila shinikizo la Madrid ambayo ndiyo klabu iliyopata mafanikio makubwa zaidi kwenye mashindano hayo, lilikuwa kubwa mno na likawazidi Bayern.
Mshambuliaji wa akiba Joselu ndiye aliyeifungia Madridmagoli mawili na kuyapindua matokeo ya mechi hiyo baada ya Alphonso Davies kuwaweka miamba hao wa Ujerumani kifua mbele mapema katika kipindi cha pili.
Kabla mabao ya Joselu, goli la kusawazisha la Madrid lilikataliwa baada ya mfungaji wa goli hilo Nacho kumsukuma Joshua Kimmich na hapo ilionekana wazi kwamba Bayern hatimaye watapambana na watani wao wa Ujerumani katika fainali.
Kosa nadra la mlinda lango
Lakini kosa lililofanywa na mlinda lango Manuel Neuer aliyeupangua mpira baada ya shuti lililopigwa na Vinicius Junior, lilimpelekea Joselu kuuelekeza mpira wavuni na kufanya mambo kuwa sawa. Dakika chache baadae beki wa kati wa Ujerumani Antonio Rudiger alimuandalia pasi safi Joselu aliyepachika wavuni bao lake la pili.
Bayern walidhani kwamba wamepata goli la kusawazisha katika muda wa ziada ila goli hilo la Mathijs de Ligt lilikataliwa kwa njia ya kutatanisha huku kulingana na kocha Thomas Tuchel, muamuzi wa mechi hiyo baadae alikiri maamuzi hayo yalikuwa ya makosa.
"Inauma, itachukua muda kurudia hali ya kawaida ila ni mechi ambayo tumejitolea na yote tumeyawacha uwanjani. Bila shaka ni vigumu kukubali ila ndio ukweli, Hakuna majuto," alisema Tuchel.
Msimu wa kuvunja moyo
Thomas Tuchel amesalia na mechi mbili tu za Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga, kama kocha wa Bayern Munich ambayo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012, imemaliza msimu mikono mitupu.
"Ninajivunia juhudi tulizoonesha leo kwasababu si rahisi kucheza hapa ila hatutoshinda chochote mwishowe, kwa hiyo hii kwa kweli si Bayern Munich, nimevunjika moyo sana msimu huu, kwa hiyo tunatumai msimu ujao tutafanya vyema," alisema Mathijs de Ligt.
Bayern kwa sasa wanatapatapa kumpata kocha atakayeichukua nafasi ya Tuchel ambaye ataondoka msimu huu utakapofikia mwisho.
Chanzo: https://www.dw.com/en/champions-league-real-madrid-stun-bayern-to-reach-bvb-final/a-69031352