1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari Ujerumani waanzisha mgomo

29 Desemba 2023

Madaktari na wataalamu wa afya Ujerumani wameanza mgomo wa siku tatu, kwa kufunga maelfu ya kliniki za matibabu kwa kile walichoeleza kuwa hali ya kipato ni ya chini na kukithiri kwa urasimu.

https://p.dw.com/p/4aiRD
Ujerumani |  Waziri wa Afya Karl Lauterbach.
Karl Lauterbach Waziri wa Afya wa Ujerumani akitoa maelezo kuhusu miradi ya kidijitali ya Serikali ya Shirikisho huko Berlin Berlin Ujerumani katika ukumbi wa Friedrichstrasse.Picha: Chris Emil Janßen/Imago Images

Maelfu ya ofisi za madaktari na kliniki hazijafunguliwa wiki hii nchini Ujerumani, wakati ambapo kunatajwa kuwepo ongezeko la janga la Corona na mafua.  

Madaktari na wataalamu wa afya wanapinga sera ya afya iiliyowekwa na serikali, wakisema imejaa urasimu, na upande wao inawaongezea gharama na kuwapunguzia kipato.

Kufuatia  sakata hilo wagonjwa wameshauriwa kutegemea zaidi huduma ya matibabu ya dharura,  wakati huu ambao vyama 20 vya madaktari navyo vikiwa vimejiunga na mgomo huo wa siku tatu.

Soma zaidiMamia ya wagonjwa waondoka hospitali ya Al-Shifa

Vyama vinavyoshiriki katika mgomo huo vimedai kuwa kufungwa kwa vituo vya kutolea huduma zaafya kunalenga kulinda maslahi mapama ya ustawi wa wagonjwa hapo baadae.

Vyama hivyo ambavyo vimeiita hatua ya sasa kama "uovu wa muda mfupi." Vinasema kuwa bajeti iliyopangwa na serikali inachochea vituo vingi kuendelea kufungwa na madaktari wengi kufikia uamuzi wa kustaafu mapema kuliko kuendelea kufanya kazi na kulipwa kipato cha chini.  

Kwa mujibu wa daktari wa magonjwa ya masikio na mwenyekiti wa chama cha Virchowbund, Dirk Heinrich ''hali jumla katika ofisi za madaktari imekuwa ya kushaajabisha kutokana na ukomo wa bajeti uiowekwa''. Dirk pia ameeleza vituo vingi havimudu gharama za kuwalipa wafanyikazi wake vile inavyopaswa, hivyo wanalazimika kupunguza baadhi ya huduma za matibabu kwa wagonjwa, na wakati mwingi wagonjwa hulazimika kusubiri kwa muda mrefu ili kuhudumiwa na madaktari wenye uwezo.

Mgomo wa madaktari kuwaathiri wazee na wasiojiweza

Akizungumza na shirika la utangazaji la umma la ZDF, Waziri wa Afya wa Ujerumani Karl Lauterbach amesema, haelewi kwa nini kuna mgomo, tena katika kipindi hiki ambacho, kuna wimbi kubwa la watu na ongezeko la magonjwa.

Waziri huyo ameeleza kuwa madai ya madaktari ya kutaka pesa zaidi yanajulikana ila mgomo hautawafikisha popote, hoja iliyoungwa mkono na  Mwenyekiti wa taasisi ya kutetea maslahi ya wagonjwa, Eugen Brysch.

Eugen amesema ''maeneo ya vijiji mgomo unawaathiri zaidi wazee na walio katika mazingira magumu. Ameshauri madaktari wawasilishe madai yao katika Wizara, ama katika makampuni ya bima, ambapo yanaweza kushughulikiwa. 

Maandamano ya kupinga kufungwa kwa hospitali  za Ujerumani yaliyofanyika Adenau, Ujerumani mnano Januari 5, 2023. Pichani ni wakaazi wa mjini na wa mashambani wa Adenau nchini Ujerumani wakipinga kufungwa kwa hospitali yao ya karibu.
Maandamano ya kupinga kufungwa kwa hospitali za Ujerumani yaliyofanyika Adenau, Ujerumani mnano Januari 5, 2023.Picha: DW

Waziri Lauterbach amesema, kuitisha pesa hachukulii kama ni kigezo, ila amefafanua kuwa suala la kurekebisha bajeti litawasilishwa kwa watendaji wa juu ili liweze kushughulikiwa.

Waziri huyo amesema katika mfumo wa huduma za afya, zipo pia taaluma zingine zenye mahitaji makubwa zaidi. Lauterbach ameiambia ZDF. kuwa sheria ya kupunguza urasimu pia imekua ikifanyiwa kazi kwa miezi kadhaa sasa.

Wizara ya Afya kukaa kikao na madaktari kujadili mustakabali wao

Wizara ya Afya, imesema mfumo wa afya Ujerumani unafanya kazi na madaktari wanalipwa vizuri, ikilinganishwa na mahali pengine barani Ulaya.  

Wizara pia imeonyesha dalili za kuafikiana na suala la madaktari ambapo Waziri wa Afya, Lauterbach ameahidi kufanya mkutano wa kilele na madaktari mwaka ujao, ili wajadili namna ya kushughulikia maswala yao.

Mfumo wa huduma za afya zisizo za hospitali nchini Ujerumani unategemea mtandao wa madaktari na wataalamu wa afya wanaoendesha shughuli zao binafsi, lakini wanalipwa na bima za afya, iwe za serikali au za binafsi. Hii ikitajwa kuwa tofauti na mfumo uliopo nchi nyingine za Ulaya.

Vyama vya madaktari, vinataka mfumo unaotumika tangu mwaka 1992 wa gharama elekezi zilizopangwa kwenye sekta ya afya ufutwe, kwa kile walichoeleza kuwa wanajikuta wanafanya kazi nyingi sawa na bure. V

yama hivyo vimetaka kuwe na aina tofauti za gharama za afya ili bima za afya nazo ziweze kusimamia malipo yao, haswa katika kipindi cha majanga na magonjwa ya mripuko.

Ongezeko la maambukizi ya COVID-19 Ujerumani