Madaktari Kenya wakataa pendekezo la kusitisha mgomo
3 Aprili 2024Baada ya wiki tatu za kuvutana na serikali kuu, hii leo madaktari wamekataa hela zilizotengwa na serikali ili kusitisha mgomo.
Hela hizo zimepangiwa kugharamia mahitaji ya madaktari wanafunzi ambao wamehitimu na bado hawajapata fursa kuanza kutoa huduma.
Soma: Mgomo wa madaktari waathiri hospitali za umma Kenya
Kwa upande wake mkuu wa idara ya huduma za umma Felix Koskei ametangaza kuwa kuanzia kesho, madaktari wanafunzi watakuwa wanakupokea barua zao za uelekezi wa hospitali watakazohudumu.
Wakati huo huo, maafisa wa utabibu nao wamejiunga na mgomo wa madaktari tangu Jumanne. Peterson Wachira ni mwenyekiti wa Chama cha maafisa wa utabibu nchini Kenya, KUCO na analalamika kuwa:
"Mwaka wa 2021 tulikuwa na mgomo na pale tukaweza kuongezewa yale marupurupu ya kuhudumu kwenye mazingira hatari kutokea shilingi alfu 3 hadi alfu 18 za Kenya. Hata hivyo hawajaweza kutupa ile hela mpaka sasa.Tuko na mkataba wa jumla, CBA, ilishindikana wakaunda kamati ya watu 3.Lakini hadi sasa hatujaona zile serikali za ugatuzi kurejea kwenye meza ndio tuseme tumekamilisha.”
Katibu mkuu wa muungano wa madaktari nchini Kenya, KMPDU, Dr Davji Atellah anashikilia kuwa kamwe hawatolegeza kamba hadi mkataba wa 2017 wa kuimarisha taaluma hiyo kutimizwa kikamilifu.Madaktari wa Kenya wakaidi amri ya mahakama na kuendelea na mgomo wao
Kauli hizo zinaungwa mkono na naibu katibu mkuu wa KMPDU Dennis Miskellah anayesisitiza kuwa wamefanya kila wawezalo ila,”Tumegoma, tumeenda mahakamani, tukaahirisha mgomo,ili waje kwenye meza ya mazungumzo wamekataa.Hatutarudi kazini, mambo ya ahadi sasa yamepita.”
Kadhalika wataalam wa maabara nao pia wamejiunga na mgomo wa madaktarihii leo. Mzozo huo wa madaktari umerejea mahakamani hii leo ili pande husika kuelezea mapya yaliyojiri mintarafu mazungumzo ya suluhu.
Jaji Byram Ongaya wa mahakama inayoshughulikia masuala ya ajira na wafanyakazi aliwapa wahusika wiki mbili za ziada kuhitimisha majadiliano.
Tayari Jaji Ongaya amewaongezea wahusika siku 14 za ziada kupata mwafaka. Serikali inasisitiza inajitahidi kama anavyoeleza naibu mkurugenzi wa afya ya umma Dr Sultan Matendechero ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa muungano wa madaktari, KMPDU na,”Tunaweza kuhimizana kuhakikisha kwa sisi sote kila mmoja anatimiza wajibu wake.Hata sisi upande wa serikali tuweze kuja na kukaa chini mezani tusingojee hadi watu waende barabarani.”Miezi mitatu ya mgomo wa wauguzi Kenya
Kwa upande wao madaktari wanataka makubaliano ya 2017 kutimizwa kabla ya kurejea kazini. Baadhi ya matakwa yao ni nyongeza ya mshahara, madaktari wanagenzi (wanafunzi) kuhudumu, mikataba kubadilika na mazingira ya kufanya kazi kuimarishwa.