Rais Macron kukutana na mameya wiki hii kufuatia vurugu
3 Julai 2023Wizara ya mambo ya ndani imesema ni watu 49 pekee waliokamatwa kufikia usiku wa manane, ikiwa ni idadi ndogo zaidi ikilinganishwa na siku zilizopita.
Ghasia zilizuka katika baadhi ya miji kama vile Lyon, ambako polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wanaharakati wa misimamo mikali ya mrengo wa kulia.
Rais Emmanuel Macron anapanga kukutana kesho na zaidi ya mameya 200 ambao maeneo yao yaliathirika na maandamano hayo ya kitaifa.
Macron pia atakutana leo na marais wa Seneti na Bunge. Jana usiku alifanya mkutano wa dharura na mawaziri wake.
Soma pia: Polisi nchini Ufaransa yawakamata zaidi ya watu 719 wakati wa ghasia za kupinga ukatili wa polisi
Ufaransa imekumbwa na vurugu na uporaji kufuatia kuuliwa kwa kupigwa risasi kijana mwenye umri wa miaka 17 na polisi wa barabarani viungani mwa mji mkuu Paris.
Bibi ya kijana huyo ametoa wito kwa waandamanaji kusitisha vurugu zao.