1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron ataka Magharibi izungumze na Putin

4 Desemba 2022

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameyataka mataifa ya Magharibi kufikiria namna ya kuyazingatia matakwa ya Urusi ya hakikisho la usalama, ikiwa Rais Vladimir Putin atakubali kuzungumzia hatima ya vita vya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4KS5r
Frankreich Emmanuel Macron
Picha: Dominique Jacovides/abaca/picture alliance

Akizungumza kwenye hotuba yake ya siku ya Jumamosi (Disemba 3), Macron alisema Ulaya inalazimika kuzitilia maanani khofu za Putin kwamba "NATO inakaribia mlangoni pake" na utumaji wa silaha ambao unaweza kuitisha Urusi, wakati ikijitayarishia mpango wake wa usalama.

Kauli ya Macron inakuja katika wakati ambapo Marekani inasema kasi ya mapigano ya Urusi nchini Ukarine inapunguwa, jambo linaloashiria huenda hali ikawa nzuri zaidi katika miezi michache ijayo.

Mkuu wa idara ya ujasusi ya Marekani, Avril Haines, amepuuzilia mbali tuhuma kwamba washauri wa Rais Vladimir Putin wamekuwa wakimzuwia kupata habari kamili za vita, akisema kwamba kiongozi huyo anajuwa vyema changamoto inayomkabili kwenye uwanja wa vita.

Shinikizo laongezeka

Mataifa ya Magharibi yanajaribu kuongeza shinikizo la kisiasa, kiuchumi na kijeshi dhidi ya Moscow, hatua ya karibuni kabisa ukiwa uamuzi wa Umoja wa Ulaya na mataifa saba yenye uchumi mkubwa zaidi duniani kuweka ukomo wa bei ya mafuta kutoka Urusi kuwa dola 60 kwa pipa.

Russland Ölfelder
Visima vya mafuta vya Urusi katika Bahari ya Caspean.Picha: Dmitry Dadonkin/TASS/Sipa USA/IMAGO

Mataifa hayo yanategemea kuwa uamuzi huo utasababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa Kremlin na kumlazimisha Rais Putin kuachana na vita vyake nchini Ukraine. 

Lakini katika hotuba yake ya usiku wa Jumamosi (Disemba 3), Rais Volodymyr Zelensky alisema hatua hiyo haitoshi.

"Sio uamuzi wenye manufaa makubwa kuweka ukomo kwa bei kwa mafuta ya Urusi, kiwango hicho kina afadhali kubwa kwa dola hili la kigaidi," alisema rais huyo, akidai kuwa bado Urusi itaweza kupata mapato ya dola bilioni 100 kwa mwaka, ambayo yatatumika kufadhili vita vyake na tawala na makundi mengine ya kigaidi.

"Fedha hizi zitatumika kuzisambaratisha nchi hizo hizo ambazo sasa zinajaribu kuepuka kuchukuwa maamuzi makini na makubwa zaidi." Alisema.

Siku ya Ijumaa (Disemba 2), Australia, Uingereza, Canada, Japan, Marekani na mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya yalikubaliana kuweka ukomo huo wa bei ya mafuta kutoka Urusi, hatua ambayo itaanza kutekelezwa Jumatatu, sambamba na vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya meli za mafuta za Urusi kwenye bahari yake.

Mamlaka nchini Urusi zimeukataa uamuzi huo na kutishia kusitisha usafirishaji wa mafuta kwa mataifa yote yaliyouidhinisha.