Macron asifu makubaliano ya kutatua mkwamo wa uhamiaji
23 Julai 2019Kulishughulikia tatizo la maelfu ya wahamiaji ambao bado wanaendelea kujaribu kuingia barani Ulaya kwa kuvuka bahari ya Mediterania, ni suala lililozua ukosoaji mkubwa hasa kutoka Italia nchi ambayo inalalamika kuwa inabeba jukumu kubwa la tatizo hilo, huku washirika wake wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wakitoa msaada mdogo sana.
Makubaliano yaliyojadiliwa jana Jumatatu, yanayolenga kufanya kazi pamoja kwa kutumia mfumo wenye ufanisi wa kugawana wahamiaji waliookolewa, yaliafikiwa katika mkutano kuhusu uhamiaji katika bahari ya Mediterania uliofanyika mjini Paris, Ufaransa.
Macron amesema mataifa 14 yameuidhinisha mpango huo, na nchi nane miongoni mwao zimekubali kushiriki kikamilifu katika kulichukulia hatua tatizo hilo.
"Hitimisho la mkutano wa asubuhi hii ni kwamba nchi wanachama 14 za Umoja wa Ulaya zimeuidhinisha waraka ulioandaliwa kwa ushirikiano wa Ufaransa na Ujerumani na kuwasilishwa na rais wa Finland huko Helsinki," amesema Macron.
Soma zaidi:Mawaziri washindwa kuafikiana kuhusu uhamiaji
Ameongeza kwamba, kati ya nchi 14, nane zimekubali kushiriki katika mfumo thabiti ambao utamruhusu kamishna kuchukua hatua kuhusu maombi na majibu ya nchi hizo nane wanachama kwa mshikamano.
Ofisi ya Macron imezitaja baadhi ya nchi hizo ambazo ni pamoja na; Ufaransa, Ujerumani, Finland, Luxembourg, Ureno, Lithuania, Croatia na Ireland, lakini sita zilizobakia hazikutajwa kwa majina.
Salvini asusia mkutano
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Matteo Salvini, ambaye haruhusu meli za uokozi za mashirika yasiyo ya kiserikali kutia nanga katika bandari zake, amesema makubaliano yatazidi kuifanya Italia kuwa kambi ya wakimbizi barani Ulaya.
Baada ya kuususia mkutano huo, Salvini amesema Italia haipokei amri na sio mshirika: kama Macron anataka kujadili suala la wahamiaji basi aende kukutana naye mjini Roma.
Mwezi uliopita, serikali ya Italia ilimkamata nahodha wa boti ya uokozi ya Ujerumani Sea-Watch 3 baada ya kuigonga boti ya Italia wakati akijaribu kutia nanga bila ya ruhusa katika bandari ya kusini ya Lampedusa.
Katika taarifa ya pamoja, shirika la kimataifa la uhamiaji IOM pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR yamesema, kazi muhimu inayofanywa na mashirika asiyo ya kiserikali lazima itambuliwe. Na mashirika hayo yasiangaliwe kama ni ya kihalifu kwa kuokoa maisha ya binadamu baharini.
Chanzo: (afp,ap)