1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron apatikana kwenye orodha ya udukuzi

21 Julai 2021

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anaongoza orodha ya viongozi 14 wa sasa na wa zamani waliolengwa katika udukuzi uliofanywa na kampuni ya Israeli ya NSO.

https://p.dw.com/p/3xmQk
Frankreich TV-Rede Macron
Picha: Ludovic Marin/AFP

Katika taarifa Katibu Mkuu wa Amnesty International Agnes Callamard amesema ufichuzi huo unastahili kuwashtua viongozi wa dunia.

Kulingana na gazeti la Washington Post, miongoni mwa namba 50,000 za simu zilizokuwa kwenye orodha ya kudukuliwa, zilizovujishwa kwa shirika la Amnesty na shirika la waandishi wa habari la Ufaransa Forbidden stories zipo pia  namba za Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Barham Salih wa Iraq.

Mfalme Mohammed wa sita wa Morocco pamoja na mawaziri wakuu walioko madarakani kwa sasa, Imran Khan wa Pakistan, Moustafa Madbouly wa Misri na Saad Eddine El Othmani wa Morocco nao pia wako kwenye orodha hiyo.

NSO inakanusha ripoti za shirika la waandishi la Forbidden Stories

Uchunguzi uliochapishwa Jumapili iliyopita na mashirika 17 ya habari ambayo ni wanachama wa shirika la habari la Forbidden Stories lililoko mjini Paris unaonyesha kuwa programu ya udukuzi  iliyotumika iliundwa na kuidhinishwa na kampuni ya Israeli ya teknolojia ya Ujasusi NSO na ilitumika katika majaribio na udukuzi wa simu za kisasa za waandishi wa habari, maafisa wa serikali na wanaharakati wa haki za binadamu.

Südafrika | Präsident Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Esa Alexander/Pool/REUTERS

Laurent Richard ni mwandishi na mwasisi wa shirika la Forbidden Stories.

"Kinachoonekana ni kwamba namba ya Rais Macron iliwekwa na mtu kutoka Morocco ambaye anaitumia kampuni ya NSO na ambaye labda alitaka kumchunguza rais wa huyo wa Ufaransa," alisema Laurent.

NSO ilitoa taarifa Jumapili ikikanusha ripoti hiyo ya vyombo vya habari ikisema imejaa uvumi na madai yasiyoweza kuthibitishwa. Kampuni hiyo ilisema pia kuwa programu yake inatumiwa tu na mashirika ya kiserikali ya ujasusi yaliyothibitishwa  na mashirika ya kulinda usalama kupambana na ugaidi na uhalifu.

Kampuni moja ya Marekani pia imegunduliwa kuwa na programu za NSO

Siku ya Jumapili pia, shirika la Amnesty lilitoa uchunguzi wa madai hayo ya udukuzi ulioonyesha mitandao ya kampuni ya Amazon ikiwa na miundo mbinu ya kampuni hiyo ya Israeli ya NSO. Baada ya hapo Amazon ilitangaza kuwa imefunga akaunti za NSO zilizoripotiwa kuhusika na udukuzi.

Kampuni nyengine iliyodaiwa kuwa na programu za udukuzi za kampuni hiyo ya Israeli ni kampuni ya Marekani Digital Ocean ambayo haikuthibitisha au kukanusha ilipoulizwa na shirika la habari la Associated Press.

Zaidi ya namba elfu moja kutoka nchi 50 zimehusishwa kwenye kadhia ya kudukuliwa na watu binafsi wakiwemo zaidi ya wanasiasa na maafisa wa serikali 600 na waandishi wa habari 189.