1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron airai Israel kuwalinda raia katika mapambano yake

9 Novemba 2023

Emmanuel Macron ameirai Israel kuwalinda raia kwenye mapambano yake dhidi ya Hamas akisema "maisha ya watu wote yana thamani" na kwamba mapambano dhidi ya ugaidi hayawezi kufanywa bila kuzingatia sheria za kimataifa.

https://p.dw.com/p/4YcrC
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/REUTERS

Macron alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa kimataifa alioutishia mjini Paris kwa dhima ya kutafuta msaada wa haraka kwa raia wa Ukanda wa Gaza wanaopitia madhila makubwa tangu kuanza kampeni ya kijeshi ya Israel ya kulitokomeza kundi la Hamas.

Macron amesema, "Mbele ya kitisho cha ugaidi, Israel inayo haki ya kujilinda.. (lakini) pia inabeba jukumu muhimu - ambalo liko wazi kwa mataifa yote ya kidemokrasi - nalo ni kuheshimu haki na kuwalinda raia wote. Kupambana na ugaidi hakuwezi kufanywa bila utaratib na Israel inalifahamu hilo.

Mkutano huo wa mjini Paris umeyaleta pamoja mataifa 50, mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya hisani, na kumetolewa ahadi kadhaa za kifedha kusaidia upatikanaji chakula, maji, vifaa vya matibabu na nishati kwa Ukanda wa Gaza.