1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Machafuko yaongezeka Ukingo wa Magharibi

29 Januari 2024

Wizara ya afya ya Palestina mjini Ramallah, imesema Wapalestina wasiopungua watano wameuawa katika operesheni tofauti za jeshi la Israel katika Ukingo wa Magharibi.

https://p.dw.com/p/4bnZQ
Machafuko katika Ukingo wa Magharibi yamzidi kuongezeka tangu vita vya Gaza vilipoanza Oktoba 7.
Machafuko katika Ukingo wa Magharibi yamzidi kuongezeka tangu vita vya Gaza vilipoanza Oktoba 7.Picha: Nasser Nasser/AP Photo/picture alliance

Kulingana na wizara ya Afya Ukingo wa Magharibi, jamaa mwenye umri wa miaka 21 aliuawa katika Kijiji cha Jenin. Wapalestina wengine wawili akiwemo wa miaka 18 waliuawa wakati wa makabiliano na wanajeshi eneo la Dura karibu na Hebron.

Kijana wa miaka 16 aliuawa katika makabiliano zaidi karibu na mji wa Jerusalem na wa tano aliuawa wakati wa makabiliano na wanajeshi karibu na mji wa Ramallah.

Jeshi la Israel liliripoti kwamba wanajeshi wake walijaribu kumkamata mshukiwa karibu na mji wa Jenin, lakini mshukiwa huyo akaanza kufyatua risasi dhidi ya wanajeshi, ndipo akapigwa risasi na kufa.

Kulingana na msemaji wa jeshi la Israel, wanajeshi wao walishambuliwa kwa mawe na silaha nyingine butu kwenye machafuko yaliyozuka usiku eneo la Dura, nao wakajibu kwa risasi za moto.

Israel yazidi kushinikizwa kusitisha mapigano Gaza

Amethibitisha kuwa watu wawili waliuawa kwenye rabsha hizo, na kwamba vurugu karibu na Ramallah bado zinachunguzwa.

Hali katika Ukingo wa Magharib imekuwa mbaya zaidi tangu vita vilipoanza kati ya wanamgambo wa Kipalestina Hamas na Israel. Vita vilivyochochewa na shambulizi la kigaidi la Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7.

Katika tukio fofauti, serikali ya Ujerumani imeshutumu wito kutoka kwa baadhi ya mawaziri wa Israel kutaka kukaliwa upya kwa Ukanda wa Gaza.

Eneo la Jenin ni miongoni mwa maeneo ambako vurugu zilishuhudiwa.
Eneo la Jenin ni miongoni mwa maeneo ambako vurugu zilishuhudiwa.Picha: Jafaar Ashitiyeh/AFP

Ofisi ya msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema miito hiyo haikubaliki kamwe, kwamba inachangia katika kuzidisha hali ya mgogoro wa sasa na inakiuka sheria ya kimataifa.

Wizara ya Mambo ya nje ya mamlaka ya Wapalestina pia imelaani vikali miito hiyo.

Mnamo Jumapili, vuguvugu la Walowezi wa Israel liliandaa kile lilichokiita "Mkutano wa Ushindi” kutaka kujengwa upya kwa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukanda wa Gaza na maeneo ya Ukingo wa Magharibi.

Guterres ayasihi mataifa kuendelea kuisaidia UNRWA

Miongoni mwa walioshiriki mkutano huo ni mawaziri kadhaa wa chama cha kihafidhina Likud, chake Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Aidha waziri wa Usalama wa Kitaifa wa Israel Itamar Ben-Gvir na waziri wa Fedha Bezalel Smotrich wanaotoka vyama vyenye marengo mikali ya kulia lakini vilivyoko kwenye serikali ya muungano ya Netanyahu pia walishiriki.

Ofisi ya msemaji wa wizara ya Mambo ya nje ya Ujerumani imepinga wazo hilo la kutanua makaazi ya walowezi Gaza na kusema suluhisho la kudumu la mzozo huo linawahitaji Wapalestina badala ya kuwaondoa Gaza.

Israel epusheni mauaji ya halaiki Gaza

Ameongeza kuwa yeyote anayefikiria kuwa anaweza kupata usalama kwa Israeli kutumia mawazo ya kuwafukuza wengine amepotea njia.

Nchi kadhaa zasitisha ufadhili kwa UNRWA

Kuhusu madai ambayo yamelitia doa shirika la misaada la Umoja wa Mataifa huko Gaza UNRWA, kwamba wafanyakazi wake walishiriki shambulizi la Oktoba 7 na wanamgambo wa Hamas dhidi ya Israel, Umoja wa Ulaya sasa unataka shirika hilo kufanyiwa ukaguzi.

Tume ya Ulaya inatarajia UNRWA kukubali kufanyiwa ukaguzi na wataalamu huru walioteuliwa na Umoja wa Ulaya na maamuzi yatatoa mweleko wa baadaye kuhusu ufadhili wa Umoja huo kwake.

Tume hiyo ya Umoja wa Ulaya imesema kupitia taarifa kwamba kwa sasa hakuna ufadhili wa ziada unaotarajiwa kwa UNRWA hadi mwisho wa Februari.

Chanzo, DPAE