Machafuko Burkina Faso, Watu milioni 2 wayakimbia makaazi
5 Juni 2023Machafuko yanayohusishwa na wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu yameisababisha Burkina Faso kuwa miongoni mwa nchi ambazo idadi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani inaongezeka kwa kasi kubwa. Takwimu za serikali zinaonesha kuwa idadi hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 2,000 tangu mwaka 2019.
Takwimu za serikali zilizotolewa mwezi Mei zilionesha kuwa zaidi ya watu milioni mbili wamelazimika kuyakimbia makaazi yao nchini Burkina Faso na kuwa wakimbizi wa ndani kwa ndani, katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Wengi wao ni wanawake na watoto, hali inayozusha hofu ya kutokea mgogoro mbaya wa kibinadamu, kwani machafuko hayo yamewasogeza mbali na mashamba yao na kuwalazimisha kurundikana katika kambi za muda mijini.
Mashirika ya kutoa misaada yanajizatiti kukabili hali hiyo ikiwemo ongezeko la mahitaji ya msaada, lakini nayo pia yanazongwa na uhaba wa fedha.
Soma pia: Burkina Faso yatangaza mpango mpana wa kupambana na mashambulizi ya itikadi kali
Moja kati ya watu wanne huhitaji msaada huku makumi ya maelfu ya watu wakikabiliwa na kitisho kikubwa cha njaa.
Uhaba wa fedha kwa mashirika ya misaada
Lakini hayo yakijiri, bado hata nusu ya dola milioni 800 ambayo ni bajeti ya misaada iliyoombwa mwaka uliopita na mashirika ya misaada haijatolewa. Hiyo ni kulingana na Umoja wa Mataifa.
Alexandra Lamarche, afisa wa ngazi ya juu katika shirika la kuwasaidia wahamiaji Refugees International, amesema "Wigo wa athari kwa watu ni mkubwa na ni mbaya katika kila hatua. Watu wengi wanaweza kufa kwa kuwa hawakupata chakula na huduma za afya, kwa sababu hawakulindwa ipasavyo na misaada ya kiutu kutoka serikalini haikutosha.
Machafuko yamesababisha mgawanyiko katika taifa hilo ambalo zamani lilikuwa la amani, na kuchangia mapinduzi mawili ya serikali mwaka uliopita.
Soma pia: Burkina Faso yaishutumu France 24 'kuwasaidia magaidi'
Viongozi wa kijeshi wameapa kupambana na ukosefu wa usalama, lakini mashambulizi yanayofanywa na wanamgambo wenye misimamo mikali ya dini ya Uislamu yamezidi kuendelea tangu Kapteni IbrahimTraore alipochukua madaraka mwezi Septemba.
Vikosi vya serikali vyadhibiti chini ya nusu ya nchi
Kulingana na takwimu za wachambuzi wa masuala ya migogoro, serikali ya Burkina Faso ina udhibiti wa chini ya asilimia 50 ya nchi hiyo, hasa maeneo ya vijijini.
Rida Lyammouri, afisa wa ngazi ya juu katika Kituo cha Sera, New South kilichoko Morocco amesema, wanamgambo wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi Al-Qaeda na Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, yanadhibiti au yanatishia maeneo makubwa.
Lyammouri ameongeza kuwa "vyombo vya usalama havina rasilimali ikiwemo wanajeshi na vifaa kuwawezesha kupambana kila kona dhidi ya makundi ya wanamgambo”.
Mkakati wa wanamgambo wa kuziba miji hivyo kuzuia usafirishaji huru wa watu na bidhaa kuingia mijini imezidisha mgogoro huo.
Soma pia: Amri ya kutotoka nje yawekwa Burkina Faso kupambana na ugaidi
Mashirika ya misaada yamesema hayo na kukadiria kuwa takriban watu 800,000 katika zaidi ya miji 20 wamezingirwa.
Wanamgambo watumia mkakati wa kuzuia usafiri kuingia miji wanayozingira
Bibata Sangli, mwenye umri wa miaka 53, ni mhamiaji aliyeukimbia mji wake wa mashariki Pama mwezi Januari mwaka 2022, kabla ya mji huo kuzingirwa. Anasema jamaa zake ni miongoni mwa watu wengine ambao bado wamekwama ndani ya mji huo wasiweze kuondoka.
Mnamo Januari mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulianza kutumia helikopta aina za Chinook kusambaza chakula katika maeneo yasikoweza kufikika kwa magari. Mfumo huo ulikuwa ghali mno, na mnamo mwezi Mei ndege hizo tatu zilipunguzwa na kubakia moja pekee. Hatua ambayo imefanya hali kuwa ngumu kuweza kuwafikishia watu walioko mbali misaada ya chakula kwa haraka.
Kadri hali ya kibinadamu inavyozidi kuzorota ndivyo uwezo wa vikundi vya misaada kufanya kazi pia unapungua.
Makundi ya kutoa misaada, wachambuzi na vilevile raia wanasema Kapteni Ibrahim Traore ambaye ni kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo analenga tu mafanikio ya kijeshi lakini hatilii maanani zaidi haki za binadamu, uhuru wa kujieleza au kuwawajibisha wanaofanya mauaji ya kiholela dhidi ya wale wanaoshukiwa kuwa wanamgambo.
Wanamgambao 50 wauawa Burkina Faso
Mnamo mwezi Aprili, vikosi vya usalama vya Burkina Faso viliwaua raia wasiopungua 150 kaskazini mwa nchi hiyo. Hayo ni kulingana na wakaazi wa Kijiji cha Karma, ambako machafuko mengi yalitokea. Waendesha mashtaka walisema wameanza uchunguzi dhidi ya mauaji hayo.
(Chanzo: APE)