1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya tabianchi na kasheshe ya Kavanaugh Magazetini

Oumilkheir Hamidou
9 Oktoba 2018

Ripoti ya baraza la kimataifa linaloshughulikia mabadiliko ya tabia nchi, na malumbano kati ya Republican na Democrats baada ya Brett Kavanaugh kuchaguliwa kuwa jaji wa korti kuu ya Marekani zahanikiza magazetini.

https://p.dw.com/p/36DHa
Symbolbilder Weltklimarat startet Beratungen zum 1,5-Grad-Ziel
Picha: picture-alliance/dpa/P. Pleul

Tunaanza na onyo la baraza la kimataifa la mabadiliko ya tabia nchi. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linasema ni jukumu la kila kiongozi kuinusuru sayari yetu. Gazeti linaendelea kuandika: "Kuzidi hali ya ujoto duniani limegeuka kuwa tatizo jumla na juhudi za kupambana na hali hiyo pia zinabidi ziwe jumla. Lakini katika enzi hizi zinazoshuhudia kuibuka viongozi wanaopigania masilahi ya kitaifa mfano wa Donald Trump, mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi haitakuwa kazi rahisi. Wenye kubisha mabadliko ya tabianchi wasiwatie ila wanasiasa wanaowajibika. Serikali zote zinalazimika kuwajibika na hasa zile za mataifa ya kiviwanda. "

Ujerumani yabidi igutuke

Gazeti la "Oberhessische Presse" linazungumzia msimamo wa serikali ya Ujerumani kuelekea ripoti ya baraza la mabadiliko ya tabianchi na kuandika: "Mabadiliko ya tabianchi hayaepukiki, madhara yake tu ndio yanayoweza kupunguzwa. Ili lengo hilo liweze kufikiwa walimwengu wanabidi wabadilishe haraka tabia zao-na hilo wataalam wa baraza la mabadiliko ya tabianchi wameliweka wazi kabisa. Serikali kuu ya Ujerumani imeonyesha kuvutiwa  na ripoti hiyo. Katibu wa dola anaeshughulikia masuala ya sayansi Michael Meister amezungumzia kuhusu "onyo"". Ni kweli hilo ni onyo lakini sio la kwanza. Hadi wakati huu serikali kuu ya Ujerumani imekuwa ikibonyeza kifungo cha kupunguza sauti kila onyo linapokuwa kubwa. Na serikali nyengine pia zinafanya hivyo hivyo. Ndio kusema hivi sasa serikali kuu ya Ujerumani itazindukana, itanyanyuka na kuwajibika?"

Kasheshe ya Kavanaugh

Kasheshe ya kuchaguliwa mwanasheria Brett Kavanaugh ajiunge na jopo la majaji tisa wa korti kuu ya Marekani inaendelea kugonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani. Kuchaguliwa kwake kunaashiria mapambano makali siku za mbele kati ya warepublican na wademocrat, linaandika gazeti la "Mittelbayerische Zeitung": "Uhasama umezidi makali kati ya wahafidhina na waliberali wa Marekani. Wawakilishi wa chama cha Democrat wanazungumzia wazi wazi kuhusu "kisasi katika uchaguzi wa baraza la Congress wiki nne kutoka sasa."Kumezuka vita" anajibu mtoto wa kiume wa Donald Trump-Donald Junior. Hakuna atakaesalimika. Baraza la Seneti limegeuka uwanja wa mapambano ya kisiasa. Mahakama  kuu ambayo kimsingi haipaswi kuelemea upande wowote imegeuzwa kitovu cha malumbano."

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri . Mohammed Abdul-Rahman