1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamno Syria: Mapinduzi mapya au masuala ya kiuchumi?

30 Agosti 2023

Kwa wiki mbili zilizopita, maandamano ya kupinga serikali nchini Syria yamekuwa yakipata nguvu. Baadhi wanasema mapinduzi mapya yanaanza nchini humo, huku wengine wakisema yanahusu watu kutaka kulisha familia zao.

https://p.dw.com/p/4Vlrt
Al-Suweida, Syria | Maandamano ya bendera za Druze
Waandamanaji kusini mwa Syria walipandisha bendera za rangi mbalimbali ya jamii ya Druze kwenye maandamanoPicha: Suwayda24/AP/picture alliance

Kwa mara ya kwanza  katika kipindi cha miaka bendera ya vuguvugu la mapinduzi nchini Syria ilionekana ikipepea katika sehemu za nchi hiyo ambazo bado ziko chini ya udhibiti wa serikali ya kiimla.

Matukio hayo ambayo hayakutarajiwa yamekuja kufuatia maandamano ya ya hivi karibuni dhidi ya serikali katika mkoa wa Kusini wa Sweida.

Syria inakabiliwa na maandamano ya kuipinga serikali ya rais Bashar al Assad katika mkoa wa Suweida ambako zaidi ya wakaazi 2000 wamekuwa wakiandamana kila uchao kwa wiki kadhaa sasa.

Nchi hiyo imekuwa katika vita tangu yaliposhuhudiwa kwa mara ya kwanza maandamano ya amani ya kudai demokrasia mnamo mwaka 2011 ambayo yalizimwa na serikali ya dikteta Bashar al Al Saad kwa nguvu kubwa za kijeshi.

Maandamano ya mwezi huu ya Wasyria katika mkoa wa Sweida  yanafanyika licha ya utawala huo wa Assad ya kujulikana wazi kwa historia yake ya  ukatili.

Idlib Syria | Maandamano dhidi ya utawala
Maandamano ya mshikamano na Sueida pia yalifanyika kaskazini mwa Syria, eneo ambalo haliko chini ya udhibiti wa serikali ya Assad.Picha: Anas Alkharboutli/dpa/picture alliance

Utawala dhaifu wa Assad

Mkaazi mmoja wa Sweida anayeshiriki maandamano hayo na ambaye jina lake tunalibana kwasababu za kiusalama, akizungumza na DW amesema hivi sasa utawala huo wa Assad uko katika hali mbaya na dhaifu na hasa katika eneo hilo.

Soma pia: Ujerumani haioni sababu ya kurejesha uhusiano na Syria

Anasema wakaazi wa mkoa huo kwa muda mrefu walikuwa wakitaka kuandaa maandamano kama yanayoshuhudiwa hivi sasa lakini vikosi vya usalama vilikuwa vikiyazuia.

Katika kipindi cha miaka 12 iliyopitautawala huo wa Assad umekuwa ukichukuwa hatua za kuwatia jela kuwatesa na hata kuwauwa wapinzani, kushambulia maeneo ya kiraia kuanzia masokoni hadi mahospitali na kuzingira na kuzinyima chakula jamii za wapinzani wa serikali.

Mkaazi wa Suweida aliyezungumza na DW anasema maandamano haya ya sasa hayawezi kuzuilika haijalishi ni kwa kiasi gani utawala wa Assad utajaribu kufanya hivyo.Amesema wako makini na wanazifahamu mbinu zote chafu na na za kihalifu za serikali ya Assad.

Mkoa huo wa Sweida ni nyumbani kwa jamii  ya Druze ambao ndio wachache nchini Syria,na barabara zote za mkoa huo za kuelekea mji mkuu Damascus zimefungwa halikadhalika ofisi za seriali na picha zote rasmi za rais Assad  zimeondolewa kwenye majengo.

As-Suwaida | Maandamano ya As-Suweida
Mjini Suweida, wenyeji pia walichora kauli mbiu za kuupinga utawala kwenye majengo ya serikali.Picha: Suwayda24/AP/picture alliance

Maandamano yasambaa kote Syria

Maandamano yamesambaa kote katika mkoa huo huku wakaazi wakifanya maandamano kiasi 50 wiki iliyopita.

Maandamano madogo ambayo ni ya kuonesha msikamano na mkoa huo wa Suweida yamekuwa pia yakishuhudiwa katika maeneo mengine ya Syria ya miji ambayo inadhibitiwa na utawala huo kama vile mji wa Daraa ulioko karibu na mpaka kati ya Syria na Jordan.

Soma pia: Moscow yaongoza kikao cha kwanza na Uturuki, Syria na Iran

Mmoja wa waandamanaji katika mji huo ameiambia DW kwamba wanashiriki maandamano hayo kwasababu serikali bado inawashikilia zaidi ya watu nusu milioni na kwasababu ya mauaji yanayofanywa na pia kwasababu ya mfumko mkubwa wa bei ya bidhaa  na kuwepo kwa vituo vya ukaguzi katika maeneo ambako wanamgambo wa serikali wanakusanya pesa kutoka kwa wakaazi wanaopita kwenye maeneo hayo.

Nae pia amesema maandamano ya sasa yataendelea mpaka pale serikali itakapoangushwa madarakani. Anasema ni maandamano ambayo hayawezi kukwepeka.

Rais Assad uso kwa uso na viongozi mataifa ya Kiarabu

Kwa upande mwingine mwanaharakati wa upinzani Radwan al Atrash anayeishi Idlib, kaskazini mwa Syria, anasema maandamano ya raia katika maeneo yanayodhibitiwa na utawala wa Assad ni muhimu sana.

Na kwa mtazamao wake anataraji kwamba maandamano ya Sweida hayatokoma na eneo zima la Kusini halitositisha maandamano mpaka watakapofikia lengo lao huku pia akiwa na matumaini kwamba maandamano hayo ya Sweida yatasambaa katika eneo zima la pwani ya Syria hadi Aleppo na mji mkuu Damascus.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW