1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUfaransa

Maandamano yaendelea Ufaransa kupinga mageuzi ya pensheni

Naomi Williams24 Machi 2023

Zaidi ya maafisa 400 vya usalama nchini Ufaransa wamejeruhiwa wakiwa wanakabiliana na waandamanaji wanaopinga mageuzi ya sera ya kustaafu na pensheni.

https://p.dw.com/p/4PCCI
Frankreich, Lyon | Proteste gegen die Rentenreform
Picha: Jeff Pachoud/AFP/Getty Images

Zaidi ya watu 450 walikamatwa jana Alhamis wakati wa maandamano hayo yaliyoanza  tangu mwanzoni mwa mwaka huu dhidi ya azma ya Rais Emmanuel Macron ya kutaka kuongeza umri wa kustaafu hadi kufikia miaka 64.

Ofisi ya rais wa Ufaransa imetangaza leo kuwa ziara ya Mfalme Charles III wa Uingereza iliyokuwa ifanyike wiki ijayo imeahirishwa baada ya vyama vya wafanyakazi kutangaza siku nyingine ya mgomo na maandamano ya kitaifa  siku ya Jumanne kudai marekebisho ya pensheni zao.

Waziri wa Mambo ya Ndani Darmanin amekiambia kituo cha CNews  kuwa kumekuwa na maandamano mengi na baadhi ya maandamano hayo yamegeuka kuwa ya vurugu, hasa katika mji mkuu  huko Paris huku akitoa takwimu za idadi ya waliokamatwa na kujeruhiwa.

Moto uliwashwa katika maeneo yanayouzunguka mji mkuu siku ya Alhamis huku makundi yenye misimamo mikali yakilaumiwa kwa kuchoma takataka ambazo hazijakusanywa na kuvunja madirisha ya maduka, na kusababisha mapigano ya mara kwa mara na polisi wa kutuliza ghasia.

Soma pia: Waziri mkuu wa Ufaransa akemea uhalifu wa waandamanaji nchini humo

Themenpaket | Streik und Proteste in Frankreich
Rais wa Ufaransa, Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/dpa/picture alliance

Zaidi ya watu milioni moja waliandamana nchi nzima siku ya Alhamisi, huku vuguvugu la maandamano likitiwa nguvu tena na mbinu na kauli za Macron za wiki iliyopita, kuhusu sheria ya kubadilisha umri wa kustaafu ambayo muswaada wake ulipitishwa na serikali bila ya kupigiwa kura na bunge wiki iliyopita na ambao umezua mzozo mwingine mkubwa wa ndani katika miezi 10 tu katika muhula wake wa pili madarakani.

Viongozi wa upinzani wajaribu kuongea na utawala

Kiongozi wa muungano wenye msimamo wa wastani wa CFDT, Laurent Berger, mapema leo akizungumza na radio ya RTL  amesema  kwamba alipata nafasi ya kuzungumza na msaidizi wa rais na kupendekeza kusitishwa kwa utekelezaji wa sheria ya pensheni kwa miezi sita, huku akisema ni wakati wa kuweka mambo sawa na huenda ndani ya miezi sita hiyo mambo yakabadilika

Wizara ya nishati mnamo jana Alhamisi ilionya kwamba usambazaji wa mafuta katika mji mkuu na viwanja vyake vya ndege ulikuwa hatarini huku safari zaidi za ndege zikikatishwa mwishoni mwa wiki hii katika viwanja vya ndege kote nchini kutokana na mgomo wa maafisa wa anga.

Soma pia: Macron ashikilia mageuzi ya pensheni kufanyika Ufaransa

Wizara ya mambo ya ndani imesema zaidi ya watu milioni moja waliandamana kote Ufaransa siku ya Alhamisi, ambapo waliojitokeza mjini Paris walikuwa 119,000, ambayo ni idadi kubwa zaidi kwa mji mkuu tangu harakati hiyo kuanza mnamo mwezi Januari.