1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Maambukizo ya Corona China yazidisha hofu duniani

3 Januari 2023

Nchi nyingi zatangaza sheria ya ulazima wa kuwapima katika viwanja vya ndege wasafiri kutoka China

https://p.dw.com/p/4LfuT
Coronavirus - Frankreich
Picha: Aurelien Morissard/AP/dpa/picture alliance

China inashuhudia ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi vya Corona baada ya kuondowa ghafla  sera yake kuumaliza  kabisa ugonjwa wa Uviko-19. Nchi nyingi ulimwenguni zimetangaza sheria mpya za kuwapima wasafiri wanaoingia kutoka China. Hata hivyo nchi hiyo imelaani hatua  hizo ikisema zinaweza kuichochea kuchukua hatua za kujibu.

Ufaransa kupitia waziri mkuu wake Elisabeth Borne leo Jumanne imesisitiza itaendelea na sheria ya kuwapima wasafiri wanaotokea China licha ya China  kulaani na kuipinga hatua hiyo. Ufaransa ni miongoni mwa nchi nyingi za ulimwengu ambazo zimeamuwa kufuata njia hiyo inayofuatwa pia na Marekani,Australia na Canada na Japan ambazo wiki iliyopita  zilisema pia zimeaanzisha utaratibu huo wa kuwapima wasafiri wanaotokea China kutokana na nchi hiyo kushindwa kuwa muwazi kuhusu takwimu za idadi ya walioambukizwa virusi vya Corona.

Italien | Corona-Tests bei Einreise aus China
Picha: Maule Maurizio/IPA/ABACA/picture alliance

Mamlaka ya afya Korea Kusini imesema nayo itaweka mpango wa lazima wa kupima wasafiri kutoka HongKong na Mcau baada ya China kufuta sera yake kali ya kupambana na virusi hivyo. Hii leo China imelaani utaratibu huo wa kuwapima wasafriri wanaotokea nchi mwake na kuonya kwamba inaweza kuichochea kuchukua hatua za kujibu. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning amedai baadhi ya nchi za Ulimwengu zimekwenda mbali zaidi katika sheria zao na kuwalenga raia wa China tu,akisema baadhi ya vitendo vinavyoendelea havikubaliki na kwamba havina  msingi wa kisayansi.

Maambukizo ya virusi vya Corona yameongezeka huko China  na mwishoni mwa mwezi Desemba nchi hiyo ilitowa ruhusu kwa watu kusafiri bila ya kuhitajika kukaa karantini hatua ambayo iliwafanya raia wake wengi kukimbilia hatua waliyoisubiri muda mrefu ya kusafiri nje ya nchi. Nchi nyingi zinalalamikia kutokuwepo uwazi kuhusu idadi ya maambukizo iliyotangazwa na serikali ya Beijing pamoja na hatari kuzuka kwa aina nyingine mpya za kirusi hicho.Ufaransa na Uingereza zatangaza ulazima wa kupima Corona kwa wasafiri kutoka China

Italien | Corona-Tests bei Einreise aus China
Picha: JENNIFER LORENZINI/REUTERS

Kwa mujibu wa China mpaka sasa ni watu 22 pekee waliokufa kutokana na Uviko 19 tangu mwezi Desemba nchini humo. Vyombo vya habari vya serikali vimeonesha kutotowa umuhimu kwa taarifa zinazozungumzia ongezeko la maambukizo,katika wakati ambapo wanasayansi wa nchi hiyo wanatarajiwa hii leo kutowa ripoti yao mbele ya shirika la afya duniani WHO,ambayo inawekewa matumaini ya kuweka wazi kwa kina data zinazohusu hali ya mabadiliko ya kirusi hicho.

Uwamuzi wa China wa kubadilisha sera yake ya kukabiliana na Corona pamoja na hatua ya kutangaza  idadi inayotiliwa shaka ya maambukizo na vifo,yote haya yamekuwa yakikosolewa ndani na nje ya nchi hiyo. Jana JUumatatu iliripoti vifo vitatu na leo gazeti rasmi la chama tawala cha China limechpisha ripoti iliyonukuu waatalamu wa nchi hiyo wakisema maradhi yanayosababisha na kirusi cha Corona athari zake sio kubwa kwa watu wengi walioambukizwa.

 

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW