1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa juu Somalia wauwawa katika shambulio la Mogadishu

3 Oktoba 2022

Watu wasiopungua tisa, miongoni mwao maafisa wa ngazi za juu kimkoa, wameuawa katika mashambulizi mawili ya kutumia miripuko ya magari Somalia. Kundi la kigaidi la al-Shabaab limetangaza kuhusika na miripuko hiyo.

https://p.dw.com/p/4Hh9g
Somalia, Mogadishu | Anschlag auf Hayat Hotel
Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Kamanda mmoja wa polisi katika mji wa Beledweyne yalikotokea mashambulizi hayo, amesema ripoti za awali zimethibitisha vifo vya watu tisa, wakiwemo waziri wa nchi na naibu mkuu wa wilaya. Kamanda huyo, Mohamed Molim Ali amesema watu wengine wapatao 10 wamejeruhiwa katika miripuko hiyo ya kujitoa muhanga, nje ya makao makuu ya wilaya.

Habari za hivi punde kutoka kwa mashahidi walio katika eneo la tukio, zimeeleza kuwa waliokufa kutokana na mashambulizi hayo ni 12. Mmoja wa mashuhuda hao, Elmi Hassan ameliambia shirika la Associated Press kwa njia ya simu kuwa aliona kwa macho yake miili ya watu iliyopatikana kwenye eneo la miripuko, akisema viungo vya binadamu vilitapakaa kila mahali.

Mashambulizi hayo ambayo kundi la al-Shabaab limedai kuhusika yamefanyika wakati serikali ya Somalia ikiimarisha shinikizo dhidi ya kundi hilo lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida. Awali leo serikali ya mjini Mogadishu imetangaza kumuuwa kamanda wa juu ya al-Shabaab Abdullahi Yare, mwanzilishi mwenza wa kundi hilo ambaye Marekani ilikuwa imetangaza zawadi ya dola milioni tatu kwa atakayewezesha kukamatwa kwake.

soma zaidi:Raia wa Somalia waombwa kuungana dhidi ya Al shabaab

Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud Picha: Feisal Omar/REUTERS

Wizara ya habari ya Somalia iliyotangaza kifo chake imesema alikuwa mhubiri  mkuu wa al-Shabaab, na kwamba kuuawa kwake kumeondoa mwiba katika jamii ya Somalia. Aidha, wizara hiyo imesema Abdullahi Yare aliaminika kuwa mrithi wa kiongozi mkuu wa al-Shabaab Ahmed Diriye ambaye duru zinasema ni mgonjwa.

Gavana wa mkoa wa Hiran, Ali Jayte Osman ambaye amenusurika shambulizi hilo amesema mripuko wa kwanza ulitokea kwenye lango la kuingia katika makao makuu ya wilaya, na baada ya dakika chache lori lilikuja kwa kasi na kuripuka karibu na jengo la ofisi za wilaya, na kuwauwa raia wengi waliokuwa wamekuja kutafuta huduma.

Rais wa Somalia aliyechaguliwa hivi karibuni, Hassan Sheikh Mohamud ameapa kutumia kila njia kulipiga vita kundi la al-Shabaab, baada ya kundi hilo kufanya msururu wa mashambulizi ya umwagaji damu, likiwemo lililoweka mzingiro wa masaa 30 kwenye hoteli ya mjini Mogadishu, ambamo watu 21 waliuawa.

Kundi hilo limekuwa likiisumbua Somalia kwa muda wa miaka 15, na licha ya kuvaliwa njuga na Umoja wa Afrika bado liko imara na linadhibiti maeneo makubwa ya Somalia.

Chanzo: ape, afpe, rtre