1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafia wa Umoja wa Mataifa wanashitakiwa kupokea rushwa

Lillian Urio9 Agosti 2005

Bwana Ben Sevan kiongozi wa zamani wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa Irak ulioruhusu nchi hiyo kuuza mafuta kwa ajili ya kununua chakula anaweza kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa kupokea rushwa.

https://p.dw.com/p/CHfO

Kamati ya kujitegemea, inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, inachunguza shtuma zilizotolewa juu ya mpango huo, imesema imegunduwa kulikuwa na malipo yasio ya halali na wanaweza kufungua mashtaka dhidi ya wahusika.

Kamati hiyo inafanya uchunguzi ni kwa kiasi gani Bwana Sevan, mzaliwa wa Syprus, alihusika na waliwakilisha ripoti yao Jumatatu iliyopita. Kamati hiyo inaongozwa na Bwana Paul Volcker, ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Benki Kuu ya Marekani.

Bwana Volcker amesema:

“Kuna ushahidi mpya na bado tuna maswali, ambayo hadi sasa hatujapata majibu tunayokubaliana nayo.”

Masaa machache kabla ya ripoti hiyo kuwasilishwa, afisa mwingine wa Umoja wa Mataifa aliyekuwa anahusika na mpango huo, wa Irak kuuza mafuta kwa ajili ya chakula, alifunguliwa mashtaka katika korti ya mjini Manhattan, huko Marekani, baada ya kungundulika kwamba alidai malipo yasio ya halali kutoka kwa kampuni iliyokuwa inaomba tenda katika mpango huo.

Umoja wa Mataifa ulianzisha mpango wa Irak kuuza mafuta kwa ajili ya chakula, wakati nchi hiyo ilikuwa imewekewa vizuizi mbalimbali, vikiwemo vya kiuchumi. Baada ya kuwekewa vizuizi hivyo Umoja wa Mataifa ilibaini kuwa wananchi wa Irak wanapata mateso ya kukosa mahitaji yao ya kila siku, ikiwemo chakula, kwa hiyo mpango huo ulianzishwa ili kuwasaidia wananchi wa Irak.

Alexander Yakovlev, wakala wa Kirusi, ndiye aliyekuwa afisa wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kufunguliwa mashtaka katika kasheshe hii.

Pia alikuwa ana shtumiwa kwa usafirishaji na utumiaji vibaya wa fedha pamoja na kupokea rushwa ya milioni moja za dola za kimarekani, kutoka kwa makampuni mengine yaliokuwa na tenda na Umoja wa Mataifa katika kazi mbalimbali.

Mwanasheria wa serikali, Bwana David Kelly, amesema Bwana Yakovlev amekubali kwamba alilipwa Maelfu ya dola za Kimarekani, kinyume na sheria, kati ya miaka ya 1993 na 2005.

Ofisi ya mwanasheria mkuu wa mji wa Manhattan bado inaendelea na uchunguzi wake dhidi ya Bwana Sevan, ambaye Jumapili iliyopita alijiuzulu kutoka kwenye nafasi yake ya Umoja wa Mataifa.

Kamati inayochunguza kesi ya Bwana Sevan imesema wanaushahidi wa kutosha dhidi yake na marafiki wengine wawili, wanaotoka Misri. Inasemekana Bwana Sevan alipokea takriban laki moja na nusu za dola za Kimarekani, kutoka kwa Marafiki hao wawili, baada ya kulipa kampuni lao tenda katika mpango huo.

Pia inasemekana kuwa marafiki hao wawili wana undugu na Bwana Boutros Boutros-Ghali, aliyewahi kuwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mara ya kwanza kamati hiyo imetoa sababa ya Bwana Sevan kujihusisha na ufisadi. Kwa mujibu wa kamati hiyo imebainika kwamba alianza kupokea malipo yasio ya halali baada ya hali yake ya kibinafsi ya kifedha kuwa ya utata.

Kwa mujibu wa afisa wa Umoja wa Mataifa Bwana Mark Brown, Katibu Mkuu wa Umoja huo Bwana Kofi Annan hafurahishwi na matokeo haya. Lakini amefurahi kwamba ripoti juu ya kuhusika kwa itatoka kabla ya mkutano mkuu wa Umoja huo utakao fanyika mwezi Septemba.

Mkutano huo utazingatia zaidi mipango ya kubadilisha mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Bwana Brown alisema:

“Je ingekuwa wewe ungependa ripoti hiyo itoke wiki mbili kabla ya mkutano mkubwa unaohusisha karibu mataifa yote ya dunia? Labda tungekuwa tunaisha katika ulimwengu mwingine. Lakini suala hili la mpango wa kuuza mafuta kwa ajili ya chakula linatokea kwenye ulimwengu wetu.”

Lakini mpango huu hauonyeshi tu makosa yanayotendeka katika Umoja wa Mataifa. Pia unaonyesha jinsi makampuni na mabenki yanavyofanya kazi kinyume na sheria.

Mwezi Oktoba wataalam wa mambo wamesema watatoa ripoti ya kiuchumi ya makampuni na mabenki 4,500. Na inasemekana takriban 2,000 kati yao hayafanyi kazi kihalali.