1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LUXEMBOURG : Mkutano wa dharura wa homa ya mafua ya ndege Ulaya

18 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEQd

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya leo wamekuwa na mazungumzo ya dharura juu ya hatari inayonyatia ya homa ya mafua ya ndege wakati Ugiriki ikichunguza kile kinachoweza kuthibitisha kuonekana kwa kirusi hakili cha homa hiyo katika nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Akiwa mwenyekiti wa mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jack Straw amesema lengo lake kuu ni kuwahakikishia wananchi kwamba kila jitihada zinafanywa kuzuwiya homa ya mafua ya ndege kujibadili kuja kuwa ile ya maambukizo ambayo inaweza kuuwa binaadamu.

Umoja wa Ulaya umetangaza kuenea kwa homa hiyo ya mafua ya ndege kutoka Asia na kuingia hadi Ulaya kuwa ni tishio la dunia lenye kuhitaji ushirikiano wa kimataifa na kuongeza kwamba Ulaya ya Magharibi haikujiandaa vizuri kukabiliana na hali ya dharura ya ugonjwa huo.

Mkuu wa masuala ya Afya wa Umoja wa Ulaya Markos Kyprianou amesema takriban nchi zote 25 wanachama wa umoja huo hazina akiba ya kutosha ya madawa ya kupambana na homa hiyo yaliyosanifiwa kwa ajili ya kukuza nguvu ya kinga kwa homa ya mafua ya kawaida kwa makundi ya watu walio rahisi kuathirika kama vile wazee,watoto,wale wenye ugonjwa wa kisukari na kadhalika.