1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Lula: Ujumbe wangu kwa Brazil ni matumaini na ujenzi

Saleh Mwanamilongo
2 Januari 2023

Lula ameapa kuwapigania watu maskini na utunzi wa mazingira na kuijenga upya nchi baada ya utawala wa kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia Jair Bolsonaro kuigawa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4LdYM
Brasilien Präsident  Luiz Inacio Lula da Silva
Picha: Ton Molina/AP Photo/picture alliance

Kurudi madarakani kwa Lula kunahitimisha kilele cha kurejea kwake katika kisiasa jambo linalowasisimua wafuasi wake na kuwakera wapinzani katika taifa lenye mgawanyiko mkali. Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Lula amesema ujumbe wake kwa Brazil ni wa matumaini na ujenzi.

''Nitatawala kwa wanaume na wanawake milioni 215 wa Brazil na sio tu kwa wale walionipigia kura. Nitaongoza kila mtu, nikiangalia mustakabali wetu mzuri wa pamoja na sio kupitia kioo cha nyuma cha migawanyiko ya zamani na kutovumiliana.",alisema Lula.

Utawala wa sheria 

Brasilien I Amtsantritt Luiz Inacio Lula da Silva
Picha: Pilar Olivares/REUTERS

Makumi kwa maelfu ya wafuasi walijipamba kwa rangi nyekundu ya Chama cha Wafanyakazi cha Lula ,wakikishangilia baada ya kuapishwa kwake. Walisherehekea wakati rais aliposema atatuma ripoti kuhusu utawala wa awali kwa wabunge wote na mamlaka za mahakama, kubatilisha amri za Bolsonaro ambazo zililegeza udhibiti wa bunduki, na kushikilia kuwa utawala wa awali umewajibika kwa ajili yake kukana na kutokukabiliana na janga la COVID-19.

Hata hivyo, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 77, alisema hana roho ya kulipiza kisasi kwa wale wanaotaka kuliongoza taifa kwa miundo yao ya kibinafsi na ya kiitikadi, lakini atahakikisha utawala wa sheria.

Wachambuzi wa siasa wanasema utawala huu wa Lula utakuwa tofauti na mihula yake miwili ya awali, hivi sasa amechukua uongozi baada ya kinyang'anyiro kikali cha urais katika zaidi ya miongo mitatu nchini Brazili na baadhi ya wapinzani wake kupinga achukuwe madaraka.

Hatua za kwanza za Lula

Brasilien I Vereidigung Luiz Inacio Lula da Silva
Picha: Jacqueline Lisboa/REUTERS

Lula ambaye ni mwanasiasa wa mrengo wa kushoto alimshinda Bolsonaro katika kura ya Oktoba 30 kwa chini ya asilimia mbili pekee. Mamia ya wafuasi wa Bolsonaro walikusanyika nje ya kambi za kijeshi tangu wakati huo, wakihoji matokeo ya uchaguzi na kuomba vikosi vya jeshi kumzuia Lula kuchukua madaraka.

Lula atalazimika kukabiliana na hali ngumu zaidi ya kiuchumi tofauti na mihula yake miwili ya mwanzo ambapo Brazil ilionyesha ushawishi wake wa kibiashara kimataifa. Katika hatua yake ya kwanza kama rais Jumapili, Lula alitia saini amri ya kukaza udhibiti wa bunduki, pia alisaini amri inayohakikisha malipo ya kila mwezi kwa familia maskini.